Putin: Urusi bado ina matumani ya mazungumzo ya amani
3 Agosti 2025Kauli hiyo inakuja huku tarehe ya mwisho ya vikwazo vipya kutoka Marekani ikikaribia, na ikionyesha kuwa hakuna mabadiliko katika msimamo wa Kremlin kuhusu vita.
Rais wa Marekani, Donald Trump, ametangaza kuwa Urusi itakabiliwa na vikwazo vipya iwapo haitasitisha mashambulizi dhidi ya Ukraine kufikia tarehe 8 Agosti. Vikwazo hivyo vitawalenga pia washirika wa kibiashara wa Moscow, hususan China na India, ambao wameendelea kununua nishati kutoka Urusi licha ya janga hilo la vita.
Shutuma za Trump kwa Putin
Trump amemshutumu vikali Putin, akiyaita mashambulizi ya karibuni ya Urusi dhidi ya Ukraine kuwa "ya kuchukiza” na kuonyesha hasira zake dhidi ya kile alichokiita "mwenendo wa kipuuzi" wa Urusi katika vita hivyo.
Hata hivyo, bila kuzungumzia moja kwa moja kauli ya Trump kuhusu muda wa mwisho, Rais Putin amesema mazungumzo ya amani yaliyofanyika hadi sasa hususan duru tatu zilizopita yameanza kuonesha dalili chanya. Zaidi alisema "Mazungumzo ni muhimu kila wakati, hasa ikiwa kuna nia ya amani. Ninayatathmini kwa mtazamo chanya. Mamia ya watu wamerudi makwao hilo ni jambo la kibinadamu. Tulikabidhi maiti za maelfu ya wanajeshi wa Ukraine, nasi tukapokea makumi kadhaa ya vijana wetu waliopoteza maisha kwa ajili ya taifa letu. Je, hilo si tukio chanya? Bila shaka ni chanya.”
Kusonga mbele kwa vikosi vya Urusi
Hata hivyo, Putin alisisitiza kuwa wanajeshi wa Urusi wanaendelea kushambulia maeneo yote ya mstari wa mbele wa mapambano, na kutangaza kuwa vikosi vya Moscow vimeuteka mji wa Chasiv Yar baada ya mapigano ya zaidi ya miezi 16. Hii ni kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Urusi iliyotolewa Alhamisi.
Ukraine, kwa upande wake, imekanusha madai hayo, ikisisitiza kuwa bado inaidhibiti sehemu kubwa ya mji huo.
Sababu za kusuasua mazungumzo ya amani
Katika miezi ya hivi karibuni, Ukraine imekuwa ikihimiza usitishaji wa mapigano mara moja, lakini Urusi imeshikilia kuwa inatafuta suluhisho la mwisho na la kudumu si makubaliano ya muda. Tangu kuanza kwa mazungumzo ya Istanbul mnamo Mei, Urusi imefanya mashambulizi ya anga kwa kiwango kikubwa zaidi, hasa dhidi ya mji mkuu Kyiv.
Serikali ya Ukraine imedai kuwa wajumbe wa Urusi walioko kwenye meza ya mazungumzo hawana mamlaka ya kufanya maamuzi makubwa. Rais Volodymyr Zelenskiy ameendelea kutoa wito kwa Rais Putin kukutana ana kwa ana kwa ajili ya mazungumzo ya moja kwa moja.