Putin: Pendekezo la kusitisha vita linahitaji tathmini zaidi
14 Machi 2025Putin amewaambia waandishi wa habari katika ikulu ya Kremlin kwamba, wanakubaliana na mapendekezo ya kusitisha uhasama na kuongeza kuwa wazo hilo liko sawa na wataliunga mkono.
Hata hivyo, kiongozi huyo wa Urusi amesema usitishaji huo unapaswa kupelekea amani ya muda mrefu pamoja na kushughulikia sababu za kimsingi za mgogoro huo.
Putin ameongeza kuwa anataka Ukraine ifutilie mbali azma yake ya kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Urusi kudhibiti kikamilifu maeneo manne ya Ukraine inayodai kuwa yake pamoja na kupunguzwa kwa ukubwa wa jeshi la Ukraine.
Pia ameweka wazi kuwa anataka vikwazo vya mataifa ya Magharibi vilegezwe na uchaguzi wa rais kufanyika nchini Ukraine, sharti ambalo Ukraine imelitaja kuwa la mapema wakati ambapo sheria ya kijeshi inatumika.