Putin atuhumiwa kufanya hila kutokutana na Zelensky
26 Agosti 2025Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz ameituhumu Moscow kwamba inaendesha kile alichokiita mkakati wa kuchelewesha hatua za kufikia makubaliano ya amani na Ukraine.
Katika mkutano na Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney mjini Berlin hivi leo, Merz amesema Rais Vladmir Putin anachelewesha makusudi juhudi za kufanyika mkutano na Rais Volodymyr Zelensky kwa lengo la kusitisha vita nchini Ukraine.
Baada ya mkutano wa hivi karibuni kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na Vladmir Putin mjini Alaska na kisha kufuatia na mkutano wa Trump, Zelensky na viongozi wa Ulaya, ilitarajiwa kwamba mkutano kati ya Putin na Zelensky ungelifuatia ndani ya kipindi cha wiki mbili.
Hata hivyo muda wa mwisho wa kufanyika mkutano huo unakaribia kumalizika siku chache zijazo na hakuna dalili ya kuitishwa kwake.
Kansela Merz amesema uamuzi anao Putin na Umoja wa Ulaya tayari unafanyia kazi vikwazo vya ziada dhidi ya Urusi.