Putin aionya Ujerumani kuipatia Ukraine makombora ya Taurus
19 Juni 2025Amesema Moscow itaizingatia hatua hiyo kuwa ni kuhusika moja kwa moja kwa Ujerumani katika vita vinavyoendelea.
Akizungumza na wahariri wa mashirika ya habari ya kimataifa kwenye mji wa kaskazini mwa Urusi wa St.Petersburg, Putin amesema ili Ukraine ifanikiwe kufyetua makombora hayo ndani ya Urusi itahitaji msaada wa kiufundi kutoka Ujerumani.
Amesema hilo litakuwa na tafsiri ya wazi kwamba maafisa wa Ujerumani wanaishambulia ardhi ya Urusi. Hata hivyo Putin amesema yuko tayari kufanya mazungumzo na Kansela Friedrich Merz ikiwa kiongozi huyo wa Ujerumani atahitaji kuwasiliana naye lakini akatahadharisha kuhusu kuvurugika kwa mahusiano kati ya Urusi na Ujerumani ikiwa hatua hiyo itafikiwa.
Matamshi hayo ya Putin yanafuatia yale yaliyotolewa mapema mwezi huu na Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius aliyesema nchi yake inafikiria kuipatia Ukraine makombora ya Taurus.
Ukraine imekuwa ikiishinikiza Ujerumani kuipatia makombora hayo yenye uwezo wa kushambulia hadi umbali wa kilometa 480 ili ijihami dhidi ya Urusi katika vita baina hayo vilivyopindukia mwaka wa tatu.