Punguzo la msaada wa USAID laathiri kaskazini mwa Kenya
15 Aprili 2025Maamuzi, yaliyochukuliwa maelfu ya kilomita kutoka Washington, tayari yameanza kuathiri shughuli katika Hospitali ya Rufaa ya Turkana katika kaunti ya Lodwar. Haya ni kwa mujibu wa kaimu mkurugenzi katika hospitali hiyo Ekiru Kidalio.
Kidalio anasema shirika la USAID lilikuwa limewaajiri wafanyakazi 64 wakiwemo wauguzi na maafisa wa kliniki, miongoni mwa wafanyakazi wapatao 400 katika hospitali hiyo.
Hatua ya kusitisha ufadhili wa USAID ni kinyume cha katiba
Kidalio ameongeza kuwa kwasasa, wafanyakazi wote wamesimamishwa kazi, shughuli zote kusitishwa na msaada wa dawa hautolewi tena. Pia ameelezea wasiwasi kuhusu uhaba wa chanjo ya ugonjwa wa Surua.
Mkurugenzi huyo amesema hafahamu kuhusu mipango yoyote ya serikali ya kenya ya kukabiliana na hali hiyo.
Gavana wa eneo hilo alihimiza hadharani kurejeshwa kwa mipango inayofadhiliwa na USAID wakati mjumbe wa Marekani Marc Dillard alipofanya ziara katika eneo hilo wiki iliyopita.
Kukatizwa kwa msaada wa USAID kwazua wasiwasi mkubwa miongoni mwa wakazi wa kaskazini mwa Kenya
Mabadiliko hayo ya kutatiza pia yamezua wasiwasi mkubwa katika eneo hilo lenye shughuli nyingi za mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa.
Lydia Muya mama wa watoto watatu mwenye umri wa miaka 32 anayeishi katika eneo hilo ambalo kulingana na takwimu za serikali, takriban asilimia 77 ya watu wanaishi katika umaskini, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba kuna wasiwasi mkubwa miongoni mwao kutokana na hatua hiyo ya Marekani ya kukatiza msaada wake.
Hali hiyo inazidi kuwa mbaya katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma ambayo inahifadhi zaidi ya watu 300,000 wengi wao kutoka Sudan Kusini, Somalia, Burundi na Rwanda.
Mwezi uliopita, maandamano yalizuka katika kambi hiyo baada ya kutolewa taarifa kwamba mgao wa bidhaa za msaada ambao tayari ulipunguzwa mwaka jana, utapunguzwa zaidi kwa sababu ya kukatizwa kwa msaada huo wa Marekani.
Marekani yakamilisha mchakato wa kufuta miradi ya USAID
Mfanyakazi mmoja wa misaada ya kibinadamu ambaye ameishi Kakuma kwa takriban miaka mitano, aliyezungumza kwa sharti la kutotambulishwa jina kwa kukosa ruhusu ya kuzungumza na vyombo vya habari, amesema ilikuwa hali ya wasiwasi huku akikadiria kuwa asilimia 40 yawafanyakazi tayari walikuwa wameachishwa kazi.
Mfanyakazi huyo ameongeza kuwa hali inaweza kuwa mbaya zaidi.
Wakimbizi wanapaswa kushughulikia kama watu na sio hali ya dharura
Wafanyikazi wa misaada wanasema faraghani kwamba hali hiyo haitokani tu na kupunguzwa kwa misaada ya Marekani lakini pia ukosefu wa mipango wa mashirika yasiokuwa ya kiserikali.
Wanasema kama wakimbizi wangeshughulikiwa kama watu na sio hali ya dharura, kukatizwa kwa misaada hiyo kusingewaathiri akimaanisha kuwa mengi zaidi yangeweza kufanywa katika mipango ya muda mrefu.