PSG yaichapa Arsenal, sasa kukutana na Inter Milan fainali
8 Mei 2025Ni baada ya kuifunga Arsenal 2 - 1 jana usiku katika mechi ya mkondo wa pili wa nusu fainali. Fabian Ruiz alifunga kombora maridadi kunako dakika ya 27 katika dimba lililofurika la Parc des Princes. Achraf Hakimi aliwafungia mabingwa hao wa Ufaransa bao la pili katika dakika ya 72 ambao dakika tatu kabla, walikuwa wamepoteza penalti kutoka kwa Vitinha.
Arsenalwalipata matumaini baada ya Bukayo Saka kutikisa wavu katika dakika ya 76 lakini muda haukutosha kwa The Gunners ambao walipoteza nafasi tatu za wazi katika dakika za mwanzo. Katika fainali ya Munich mnamo Mei 31, PSG watakutana na mabingwa mara tatu Inter Milan, walioshinda nusu fainali ya kukata na shoka kwa jumla ya mabao 7-6 dhidi ya Barcelona siku iliyotangulia.
PSG wanaomilikiwa na Qatar walicheza fainali ya 2020 na kupoteza kwa Bayern Munich, na pia waliondolewa katika nusu fainali kadhaa baada ya hapo.