PSG na Tottenham kukwaana katika Super Cup
13 Agosti 2025Mechi hiyo kwa kawaida huchezwa mwanzoni mwa msimu na inawapatanisha mabingwa wa Ligi ya Vilabu Bingwa Ulaya na mabingwa wa Ligi ya Ulaya na PSG wanaingia kwenye mechi hii kama timu inayopigiwa upatu pakubwa.
PSG walishinda makombe matatu msimu uliopita ikiwemo kushinda Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza na watakuwa wanatafuta kurudi katika mazoea yao ya ushindi baada ya kulazwa na Chelsea katika fainali ya Kombe la Dunia la Vilabu huko Marekani.
Tottenham kwa upande wao walifikisha mwisho wao ukame wa makombe walipoishinda Manchester United kwenye fainali ya Ligi ya Ulaya na kushinda kombe la kwanza katika kipindi cha miaka 17.
Spurs wana kocha mpya, Thomas Frank, ila pia wanawakosa baadhi ya wachezaji muhimu akiwemo James Maddison na Dejan Kulusevski ambao wamejeruhiwa na nyota wa muda mrefu Son Heung Min akiwa aliihama klabu hiyo na kutimkia Marekani katika klabu ya LAFC.
Hii ndiyo mara ya kwnaza kwa Spurs kushiriki Super Cup huku PSG wakiwa waliwahi kushiriki mwaka 1996 ambapo walilazwa na Juventus kwa jumla ya mabao 9-2 katika mechi iliyochezwa kwa mikumbo miwili.