Polisi ya Minneapolis kufanyiwa mageuzi
8 Juni 2020Kifo hicho kilisababisha maandamano makubwa kote nchini Marekani. Pamoja na jiji hilo, majiji mengine pia nchini humo yametangaza hatua za mageuzi ndani ya jeshi la polisi.
Wajumbe tisa kati ya 13 wa halmashauri ya jiji la Minneapolis wameahidi hapo jana kuivunja idara hiyo, na kuunda njia mpya ya kuhakikisha usalama wa umma, hatua ambayo haikutarajiwa hata kidogo wiki mbili tu zilizopita.
Mmoja wa wajumbe wa baraza hilo Jeremiah Ellis ameandika kupitia ukurasa wake wa twitter kwamba wataivunja idara ya polisi ya Minneapolis na kabla ya kuiunda upya watafikikiria kwa kina namna ya kushughulikia suala la usalama wa raia na masuala ya dharura.
Vuguvugu la awali la kushinikiza jeshi la polisi kupunguziwa bajeti lilianza kabla ya maandamano ya hivi karibuni, lakini sasa limepata uungwaji mkono mpya kufuatia video iliyomuonyesha afisa wa polisi Derek Chauvin akiikandamiza kwa goti shingo ya mmarekani mweusi George Floyd ambaye hakuwa na silaha mwezi uliopita.
Bado majadiliano rasmi kuhusu hatua hizo.
Halmashauri ya Minneapolis hata hivyo bado haijajadiliana rasmi kuhusu kupunguza bajeti ya idara hiyo ya polisi ama hata kiliunda upya. Lakini rais wa halmashauri hiyo Lisa Bender amekiambia kituo cha televisheni cha nchini humo cha CNN kwamba wengi walikuwa wanaunga mkono hatua hizo, ingawa hilo si suala la muda mfupi. Mjumbe wa halmashauri hiyo Phillippe Cunningham alisema "Kwa hiyo kuna fursa kwetu sisi kuangazia hatua inayofuata.. lakini kwa kweli tutaipunguza sana bajeti ya mwaka 2021."
Viongozi wa kuchaguliwa katika majiji ya New York na Los Angeles wamesema watapunguza bajeti za idara za polisi ili kuangazia namna ya kuzielekeza kwenye huduma za kijamii, ishara inayoonyesha kwamba vuguvugu hilo sasa linapata nguvu zaidi. Mjini New York, Meya Bill de Blasio alitangaza msururu wa mageuzi aliyosema yameandaliwa ili kujenga kuaminiana kati ya raia wa jiji hilo na idara ya polisi.
Maandamano makubwa mwishoni mwa wiki iliyopita kote nchini Marekani kwa kiasi kikubwa yalikuwa ya amani. Mmoja wa maveterani mweusi wa jeshi la anga nchini humo Nikky Williams alinukuliwa akisema kwenye maandamano hayo mjini Washington hapo jana kwamba kuna polisi kwenye familia yake na ana imani na uwepo wao. Lakini hata hivyo amesema ni lazima kufanyike mageuzi.
Mashirika: AFPE/RTRE