Polisi wa Ujerumani wawasaka washukiwa wa mauaji ya Nauheim
21 Aprili 2025Polisi wa Ujerumani katika mji wa Nauheim kaskazini mwa Frankfurt Jumapili walitanua msako wa kumtafuta mshukiwa mwingine mmoja ambaye hajulikani aliko baada ya wanaume wawili raia wa Uturuki kupigwa risasi na kuuliwa siku moja kabla.
Polisi wa eneo la Hesse walisema jana Jumapili kwamba wahanga hao wawili walipigwa risasi katika eneo la makazi la Bad Nauheim, kiasi kilometa 35 kaskazini mwa mji wa Frankfurt na sababu haikufahamika mara moja.
Shirika la habari la Ujerumani DPA limesema mamlaka hawafutilii mbali uwezekano kwamba washukiwa zaidi ya mmoja huenda walihusika na uhalifu huo unaoonekana kuchochewa na sasabu za kibinafsi.
Likivinukuu vyanzo vya polisi na waendesha mashitaka, shirika hilo limesema watu hao ni baba mkwe aliyekuwa na umri wa miaka 59 na mkwe wake wa umri wa miaka 28.
Kwa mujibu wa gazeti la Hesseschau linalochapishwa katika eneo hilo, kikosi kikubwa cha polisi kilitumwa kufanya msako kufuatia mauaji hayo ya risasi Jumamosi iliyopita.