Polisi wa mauaji ya Floyd aachiwa kwa dhamana
11 Juni 2020Mmoja wa polisi wanne wa zamani waMinneapolis walioshitakiwa kusababisha kifo cha George Floyd ameachiwa kwa dhamana hapo jana, huku kaka wa Floyd, Philonise Floyd akiwatolea mwito wa huzuni wabunge wa Marekani kuzuia maumivu na kupitisha mageuzi yatakayowawajibisha polisi kutokana na ukatili wanaoufanya.
Afisa huyo wa zamani wa polisi, Thomas Lane ameachiwa kwa dhamana ya dola 750,000 kutoka gereza ya kaunti ya Hannepin alikokuwa anashikiliwa. Alikuwa miongoni mwa maafisa watatu walioshutumiwa kwa kusaidia na kushawishi mauaji ya bila kukusudia ya Floyd Mei 25.
Maafisa wote wanne wamefukuzwa katika idara ya polisi ya Minneapolis. Wakili wa Lane, Earl Gray hakupatikana mara moja kwa njia ya simu, alipotafutwa na shirika la habari la Reuters jana usiku, lakini hata hivyo aliwaambia waandishi wa habari kwamba mteja wake alikuwa akijaribu kumsaidia Floyd.
Wakili wa Derek Chauvin, polisi wa zamani ambaye ni mshukiwa mkuu katika mauaji ya Floyd, pia hakupatikana mara moja kuzungumzia hatua hiyo.
Hapo jana, kaka wa Floyd, Philonise Floyd aliwatolea mwito wa huzuni wabunge wa bunge la Marekani akiwaomba kuzuia maumivu na kupitisha mageuzi yatakayowawajibisha polisi kutokana na ukatili wao.
Siku moja baada ya kumzika kaka yake mjini Houston, Philonise alijitokeza mbele ya kikao cha bunge, ambako alielezea machungu anayoyapata akiitazama video iliyoonyesha kifo cha George na kuwataka wabunge kuchukua hatua za kurekebisha changamoto zinazojitokeza wakati wa utekezaji wa sheria, ikiwa ni pamoja na ubaguzi wa kimfumo.
"Imetosha. Watu wanaoandamana wanawaambia 'imetosha'. Watu waliwachagua mzungumze kwa niaba yao na kufanya mabadiliko chanya. Jina la George linamaanisha kitu. Mna fursa hapa leo ya kufanya majina yenu yakamaanisha kitu pia. Ikiwa kifo chake kitaishia kuubadilisha ulimwengu kuwa bora - na nadhani itakuwa - basi alikufa kama alivyoishi. Ni juu yako kuhakikisha kuwa kifo chake hakikuwa bure" alisema Philonise
Spika wa bunge Nancy Pelosi katika hatua nyingine ametaka sanamu za viongozi wa majimbo ya Marekani yaliyounga mkono utumwa, kama ya Jefferson Davis kuondolewa katika jengo la bunge la Capitol Hill. Pelosi ameiambia kamati ya seneti yenye mamlaka ya kisheria kuhusu suala hilo tete, akisema sanamu hizo zinahimiza chuki na wala si turathi.
Hatua hii inakuja wakati tayari sanamu zinazoashiria ubaguzi zikiangushwa, kuharibiwa ama kuondolewa na waandamanaji katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na sanamu la Christopher Columbus mjini Boston na sanamu ya Edward Colston aliyekuwa mfanyabiashara wa watumwa, katika karne ya 17.
Mashirika: AFPE/RTRE/APE.