Polisi Ujerumani watoa tahadhari, watoto kuuzwa mtandaoni
28 Agosti 2025Mamlaka nchini Ujerumani zimekamilisha uchunguzi wa idadi kubwa zaidi ya kesi za usafirishaji haramu wa binadamu na unyanyasaji mnamo mwaka 2024 tangu matukio hayo yalipoanza kuorodheshwa mnamo mwaka 2000.
Maafisa hao wa uchunguzi, wamebainisha matukio mengine ya kusikitisha ya watoto kuuzwa mtandaoni.
Polisi wa Ujerumani wanaoshughulikia visa vya jinai (BKA) huko Wiesbaden, wamesema Alhamisi kwamba uchunguzi wa matukio 576 uliokamilishwa mwaka jana, umeonesha kuna ongezeko la asilimia 13 la mikasa hiyo ikilinganishwa na makosa ya jinai yaliyofanywa mwaka wa 2023.
Katika zaidi ya matukio 200, watoto na vijana wanaobaleghe waliorodheshwa kama waathiriwa wa maonevu, huku watoto wengine 195 wakiwa wamenyanyaswa kingono.
BKA imesema sababu mojawapo ya ongezeko la kadhia hiyo miongoni mwa sababu zingine ni kukosekana mifumo ya kutosha ya ulinzi kwenye majukwaa ya mitandao, hali inayochochea unyanyasaji wa watoto wanapotumia intaneti.