Helikopta ya Umoja wa Afrika yapata ajali Somalia
2 Julai 2025Helikopta hiyo ilikuwa sehemu ya kikosi cha Umoja wa Afrika cha kufanikisha utulivu Somalia AUSSOM, kilichokuwa na jukumu la kupambana na kiundi la wanamgambo wa Al Shabaab.
Uganda kupitia msemaji wa jeshi Felix Kulayigye imethibitisha kumiliki ndege hiyo iliyoanguka mapema leo asubuhi katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Aden Abdulle mjini Mogadishu ikitokea kambi ya jeshi ya Baledogle.
Maafisa watatu kati ya nane waliokuwepo katika helikopta hiyo waliokolewa mara moja na wanapokea matibabu katika hospitali ya AUSSOM. Hakuna taarifa zaidi zilizotolewa kuhusu manusura hao.
Kundi la waokoaji waliripotiwa kuwepo katika tukio la ajali kujaribu kuwaokokoa maafisa wengine na kutoa miili ya walioangamia. Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka ya usafiri wa anga nchini Somaia Ahmed Moalim Hassan, amesema wanafanya uchunguzi wa kubaini sababu ya ajali hiyo. Amethibitisha pia kuwa shughuli katika uwanja huo wa ndege inaendelea kama kawaida.