Polisi Kenya yathibitisha kushikilia Boniface Mwangi
20 Julai 2025Idara ya upelelezi nchini Kenya, DCI imesema katika mtandao wake wa X kwamba maafisa wake wamemkamata Mwangi nyumbani kwake katika kaunti ya Machakos na kupata mabomu mawili ya kutoa machozi, mkanda wa risasi, simu mbili za mkononi, kompyuta na vijitabu kadhaa vya kutunza kumbukumbu.
Kando na madai ya ugaidi, Boniface Mwangi pia anapaswa kusimamishwa kizimbani kujibu makosa ya kumiliki silaha kinyume cha sheria. Mwakilishi wake hakuweza kupatikana mara moja kutoa maoni juu ya ripoti hii.
Mtu mmoja amejeruhiwa katika maandamano ya kupinga serikali Kenya
Taarifa za kukamatwa kwake tayari zimezua hasira miongoni mwa wakenya katika mitandao ya kijamii, huku wengi wakitaka mwanaharakati huyo kuachiwa huru mara moja.
Vijana wa kenya maarufu kama Gen Z waliokasirishwa na hali ya uchumi kudorora nchini humo wamekuwa wakiandamana mara kwa mara kupinga hali hiyo, rushwa na vitendo vya ukatili wa polisi dhidi yao.
Vijana hao wamekuwa wakitaka mageuzi serikalini ikiwa ni pamoja na kumtaka rais Ruto kun'gatuka madarakani.