PLO yapiga kura kuunda nafasi ya makamu wa rais
25 Aprili 2025Chama cha Ukombozi wa Palestina (PLO) limepitisha hatua ya kihistoria kwa kupiga kura kuanzisha nafasi ya Makamu wa Rais, hatua inayotafsiriwa na wachambuzi kama njia ya kumtayarishia mrithi kiongozi wa muda mrefu wa Palestina, Mahmoud Abbas.
Taarifa hizi zilitolewa Alhamisi na mjumbe wa baraza kuu la PLO, Rizq Namoura, kupitia mahojiano na runinga ya Palestina. Alisema kuwa uamuzi huo uliungwa mkono kwa karibu kauli moja. Shirika rasmi la habari la Palestina,Wafa, pia lilithibitisha kupitishwa kwa pendekezo hilo.
Hatua hii imekuja baada ya miaka mingi ya mashinikizo ya kimataifa yanayohitaji mageuzi ndani ya taasisi za Palestina, hasa wakati huu ambapo mataifa ya Kiarabu na nchi za Magharibi zinatamani kuona Mamlaka ya Palestina (PA), inayoongozwa pia na Abbas, ikichukua nafasi kubwa katika utawala wa Gaza baada ya vita.
"Mfumo wa kisiasa wa Palestina tayari ni dhoofu sana"
Aref Jaffal, mchambuzi wa siasa na mkurugenzi wa Kituo cha Ufuatiliaji wa Uchaguzi cha Al-Marsad, alisema nafasi hiyo mpya ni njia ya maandalizi ya urithi wa Abbas, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 89. "Mfumo wa kisiasa wa Palestina tayari ni dhoofu sana. Hivyo, naamini kuwa mipango hii yote inalenga kumtayarisha mrithi wa Abbas," alisema Jaffal.
Katika mkutano wa kilele uliofanyika Cairo mwezi Machi kuhusu mustakabali wa Gaza, Abbas alikuwa ametangaza nia ya kuanzisha wadhifa wa Makamu wa Rais ndani ya PLO, ambayo yeye ni mwenyekiti wake. Tangu kuchaguliwa kuwa Rais wa PA mwaka 2005 baada ya kifo cha Yasser Arafat, Abbas hajawahi kukabiliwa na uchaguzi mpya wa rais licha ya kipindi chake cha miaka minne kukamilika mwaka 2009.
Wasiwasi wa vyama vya Palestina na lawama kwa mataifa ya Magharibi
Licha ya hatua hiyo mpya, mkutano wa PLO unaoendelea mjini Ramallah umeibua upinzani mkali kutoka kwa baadhi ya vyama vya Palestina. Kundi la Hamas limeukosoa mkutano huo likisema kuwa "unazidisha mgawanyiko, unaendeleza maamuzi ya upande mmoja na kuwakatisha tamaa wananchi wa Palestina wanaotamani umoja.
"Vyama kadhaa kutoka Ukingo wa Magharibi vilijiondoa kwenye mkutano huo mara baada ya pendekezo la kuanzishwa kwa wadhifa wa Makamu wa Rais kuwasilishwa. Miongoni mwao ni chama cha Democratic Front for the Liberation of Palestine(DFLP), ambacho kilieleza kuwa kikao hicho kiliitishwa kwa shinikizo kutoka mataifa ya Magharibi, hasa Marekani.
"Hatua hii inatishia uhuru wa PLO na ni dalili ya kuingiliwa kwa ajenda ya Palestina na mataifa ya nje," alisema Ramzi Rabah kutoka DFLP. Chama cha Popular Front for the Liberation of Palestine (PFLP) pia kilijiondoa kikidai kuwa ajenda ya mageuzi haijafanyiwa mashauriano ya kina.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Wafa, kati ya wanachama 188 wa baraza kuu la PLO, 170 waliunga mkono pendekezo la kuanzisha nafasi ya Makamu wa Rais.
Mageuzi ya kisiasa yakichochewa na hali ya kifedha na mashinikizo ya wafadhili
Hali ya kifedha ya PA imezorota mno, na tangu shambulio la Hamas dhidi ya Israel lililosababisha vita vya Gaza, wafadhili wa kimataifa wamezidi kusisitiza kuwa misaada yao itatolewa tu iwapo kutakuwa na mageuzi ya kweli ya kisiasa na taasisi.
Jumatano, Abbas alisisitiza kuwa kuanzishwa kwa wadhifa wa Makamu wa Rais kutaimarisha taasisi za Palestina na kusaidia kupanua utambuzi wa kimataifa wa taifa la Palestina.
Baadhi ya wachambuzi hata hivyo wanaamini kuwa Abbas anajaribu tu kuonyesha kwamba anagawa madaraka, bila kuachia ushawishi wake halisi.