PARIS:Wafanya fujo wachukuliwe hatua kali
5 Novemba 2005Nchini Ufaransa,vijana kutoka familia za wahamiaji wa Kiafrika wameendelea kufanya ghasia kwa usiku wa tisa kwa mfululizo.Usiku wa kuamkia jumamosi machafuko yalishika kasi ukingoni mwa mji mkuu Paris na miji mingine.Kwa mujibu wa ripoti ya polisi takriban magari 900 yamechomwa moto na idadi kubwa ya majengo yameharibiwa au yameteketezwa kabisa.Zaidi ya watu 259 wanaoshukiwa kuhusika na machafuko hayo wamekamatwa na walinzi wa usalama.Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa,Nicolas Sarkozy kutoa amri ya kuwakamata watu wanaofanya ghasia.Machafuko yalianza wiki iliyopita baada ya vijana wawili wenye asili ya Afrika ya Kaskazini,kufariki kwa umeme walipoparamia ukuta wa kinu cha kusafirisha umeme.Wenyeji wa eneo hilo wamesema kuwa vijana hao walikuwa wakiwakimbia polisi,lakini hayo yamekanushwa na polisi.