Papa Leo XIV atoa wito wa kusitishwa kwa vita vya Gaza
27 Agosti 2025Papa Leo ameutoa wito huo siku ya Jumatano wakati akiwahutubia waumini huko Vatican akitaka kusitishwa kwa vita huko Gaza na kuachiliwa kwa mateka wa Israel ambao bado wamesalia mikononi mwa Hamas:
" Natoa wito wa kuachiliwa kwa mateka wote na kufikiwa kwa usitishaji wa kudumu wa mapigano. Pia misaada ya kibinadamu iweze kuingia kwa usalama, na sheria ya kibinadamu iheshimiwe kikamilifu, hasa wajibu wa kuwalinda raia, marufuku ya adhabu ya pamoja, matumizi ya nguvu kiholela na watu kulazimishwa kuyahama makazi yao."
Wito huo wa Kiongozi huyo Mkuu wa Kanisa Katoliki umetolewa wakati jeshi la Israel likiwa limezidisha mashambulizi yake katika mji wa Gaza licha ya miito ya kimataifa kuongezeka ikihimiza vita hivyo vikomeshwe.
Jeshi la Israel limethibitisha kuwa vikosi vyake vinaendelea na operesheni nje kidogo ya mji wa Gaza ili kusaka na kusambaratisha kile walichokiita miundombinu ya kigaidi iliyodhahiri na iliyofichwa chini ya ardhi.
Msemaji wa jeshi la Israel Avichay Adraee, ameandika kwenye ukurasa wa mtandao wa kijamii wa X kwamba kitendo cha kuhamishwa kwa Wapalestina kutoka katika mji huo wa Gaza ni jambo lisiloweza kuepukika.
Idadi kubwa ya wakazi wa Gaza wameyakimbia makazi yao angalau mara moja katika vita hivi, na mashirika ya misaada yanayofanya kazi Gaza yamekuwa yakitahadharisha kwamba mpango huo wa Israel wa kuwahamisha karibu watu milioni moja kutoka mji wa Gaza hautekelezeki na ni hatari sana.
Serikali ya Netanyahu yaendelea kukosolewa
Serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu imekuwa ikikabiliwa na ukosoaji na miito inayoongezeka ndani na nje ya Israel, ikitaka kukomeshwa kwa vita hivyo vilivyosababisha maafa makubwa.
Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni, amelaani mashambulizi ya Israel huko Gaza akisema hayana uwiano huku akisisitiza kuwa vita hivi vya karibu miaka miwili vimesababisha maafa kwa wahanga wengi wasio na hatia.
Yote hayo yakiarifiwa, baadaye Jumatano jioni Rais wa Marekani Donald Trump anatarajia kuwa mwenyeji wa mkutano huko Washington utakaojadili mipango ya baada ya vita huko Gaza.
Mjumbe maalum wa Marekani kwa Mashariki ya Kati Steve Witkoff amedokeza kuwa Marekani inatarajia kupatia suluhu vita hivyo vya Gaza kufikia mwishoni mwa mwaka huu, lakini hadi sasa juhudi za upatanishi zinazosimamiwa na Qatar, Misri na Marekani zimeonekana kukwama.
//DPA, AP, Reuters, AFP