Papa Leo XIV ahimiza diplomasia katika kusuluhisha mizozo
30 Julai 2025Papa Leo ameitoa kauli hiyo alipokuwa akiadhimisha miaka 50 ya Makubaliano ya kihistoria ya Helsinki, yaliyosainiwa enzi ya Vita Baridi ambayo yalianzisha enzi mpya ya usalama na haki za binadamu.
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki amesema Agosti 1 ni siku ya kumbukumbu ya kuhitimishwa kwa mkutano wa kilele wa mataifa 35 nchini Finland, ambao ulikuwa nguzo ya uwepo wa amani duniani huku akisisitiza kuendelea kuheshimu makubaliano hayo.
"Leo, kuliko wakati wowote ule, ni muhimu kuenzi makubaliano ya Helsinki, kuendeleza mazungumzo, kuimarisha ushirikiano na kuifanya diplomasia kuwa njia inayopewa kipaumbele katika kuzuia na kutatua migogoro."
Katika kilele cha Vita Baridi kwenye miaka ya 1970, Rais wa Finland wakati huo Urho Kekkonen aliandaa mkutano wa kilele kati ya Marekani na Umoja wa KiSovieti ambapo Rais wa Marekani Gerald Ford, kiongozi wa KiSovieti Leonid Brezhnev na wengine walitia saini makubaliano ya kihistoria kwa ajili ya amani, kuboresha uhusiano kati ya Mashariki na Magharibi, kuimarisha usalama wa Ulaya na haki za binaadamu.