Papa Leo: Sheria za kimataifa ziheshimiwe Mashariki ya Kati
27 Juni 2025Papa Leo, ametoa tamko hilo mjini Vatican alipokutana na maaskofu na viongozi wa mashirika ya misaada kutoka eneo la Mashariki ya Kati.
Akionekana kutumia lugha yenye mchanganyiko wa mafumbo katika kikao hicho Papa Leo amesema kwamba mataifa ya ukanda huo yameathiriwa vikali na vita vya mara kwa mara vinavyosababisha mataifa hayo kupokonywa haki zao za msingi kwa maslahi ya kisiasa huku eneo zima likiendelea kufunikwa na wingu zito la chuki ambalo limechafua hata hewa wanayovuta.
"Leo hii, mzozo huu mkali unaonekana kushika kasi nyingine katika kiwango cha kibaya kabisa ambacho hakijawahi kushuhuduwa hapo awali” Alisema Papa Leo huku akiongeza kuwa hali ya wapalestina katika ukanda uliozingirwa wa Gaza inasikitisha na inayokiuka hadhi ya binadamu kabisa.
Aomba wahusika kumpa Mungu nafasi wakati wanaposaka suluhu
Akionekana kusikitishwa na kile kinachoendelea kutokea katika eneo la mashariki hasa Gaza Papa Leo ameomba uwepo wa Mungu kwa kuwapa masikio ya kiroho wale wenye kuhusika na utatuzi wa mzozo huo.
"Na iwe sauti hii inayotoka kwa Aliye Juu iweze kusikika. Na madonda yaliyosababishwa na vitendo vya umwagaji damu katika vita hivi yakaponywe. Na njia za mazungumzo, diplomasia na amani zipewe nafasi," alisema Papa Leo.
Papa Leo, ambaye alichukua nafasi ya upapa tarehe 8 Mwezi wa tano baada ya kifo cha Papa Francis mwezi uliopita pia ameitaka Israel kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingia Gaza, hata hivyo katika kikao hicho Papa Leo aliepuka kuitaja Israel moja kwa moja.
Kiongozi huyo wa Kanisa katoliki duniani Papa Leo, mzaliwa wa Marekani pia hakuvizungumzia vita vya siku kumi na mbili kati ya Israel na Iran ambapo Marekani pia ilishambulia maeneo yaliyodhaniwa kuhifadhi vinu vya nyuklia vya Iran.
"Ni suala la kusikitisha sana kuona kanuni ya ‘mwenye nguvu ndiyo sahihi' ikitawala katika mizozo mingi inayoendelea sasa, haya yote yakiwa ni kwa ajili ya kuhalalisha na kufakinisha mkakati unaolinda maslahi binafsi,” alisema Papa Leo
Aliongeza kusema kwamba inasikitisha na inatia hofu kuona nguvu ya sheria za kimataifa na sheria za kibinadamu za kimataifa zimechukuliwa na sera za kuwalizimisha wengine kwa ajili ya maslahi fulani.