Papa Leo alaani mfumo wa kiuchumi unaowatenga watu maskini
18 Mei 2025Ameyaeleza hayo wakati wa mahubiri yaliyotolewa mbele ya viongozi wa ulimwengu akiwemo Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance. Papa Leo ameongoza misa yake ya kwanza rasmi katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, siku kumi baada ya kuchaguliwa kuwa kiongozi wa Wakatoliki bilioni 1.4 kote ulimwenguni.
Alianza shughuli za siku kwa kuzunguka akitumia gari lake jeupe maalumu kwa Papa huku akitabasamu na kuwapungia mkono na kuwabariki makumi ya maelfu ya watu waliohudhuria ibada hiyo mjini Vatican. Kwenye hotuba yake, alitoa mwito kwa Kanisa kuwa nguvu ya mabadiliko katika ulimwengu wa migawanyiko na chuki.
Leo ameandika historia kuwa papa wa kwanza kutoka Marekani, na nchi yake iliwakilishwa na Vance, aliyejiunga na Ukatoliki mnamo mwaka wa 2019, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio ambaye pia ni Mkatoliki.