PAPA JOHN PAUL WA PILI MIAKA 25 ya UPAPA
15 Oktoba 2003
Katika miaka yake 25 katika wadhifa wa Upapa John Paul wa Pili amezitembelea nchi nyingi za Amerika ya Kusini na Carribean na safari zake zimebadili sura ya Kanisa la Roma la Kikatoliki katika eneo hilo na kuliweka kando kundi lake lenye mtizamo wa mageuzi ambalo liliwahi kuja juu wakati fulani.
Mwishoni mwa mwezi wa Septemba papa alizidisha idadi ya makadinali wa Amerika ya Kusini kutoka 21 na hadi kuwa 24 uamuzi ambao wachunguzi wa mambo wanautafsiri kuwa ni hatua nyengine ya kuimarisha nadharia ya kuwaweka viongozi wa kidini kwa kuzingatia maeneo wanakotoka katika eneo hilo lenye wafuasi wengi wa dhehebu la Kikatoliki wakati hali ya afya yake ikizidi kuzorota.
Papa mwenye umri wa miaka 83 anasumbuliwa na ugonjwa wa kutetemeka na ule unaoathiri viungo na hivi karibuni amekuwa pia akipata tabu kuzungumza.
Takriban maaskofu wote wazee 184 na wengine wapya 31 ambao kuanzia mwezi huu wataunda Baraza la Maaskofu Wakuu wanafuata msimamo wa sasa wa nadharia ya Vatikani.Kwa ujumla wao 135 kati yao wana umri ulio chini miaka 80 na kwa hiyo wanastahiki kutangazwa kumrithi Papa John Paul wa Pili iwapo atajiuzulu au atafariki katika kipindi cha miezi sita ijayo.
Karol Wojytla amezaliwa nchini Poland na amechaguliwa kuwa papa hapo tarehe 16 mwezi wa Oktoba mwaka 1978.Tokea wakati huo amefunga safari 16 kuvuka Bahari ya Atlantiki na kuelekea Amerika ya Kusini na Carribean.Mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 1979 ziara ambayo ilijumuisha Santo Domingo,Mexico na Bahamas.Mara ya mwisho ilikuwa ni mwaka 2002 wakati aliporudi tena Mexico na kuitembelea pia Guatemala.
Katika misafara hiyo alitowa chakula cha bwana kwa madikteta,aliwahushutumu Marais na kuwaweka kwenye nadhari watu wanaolikashifu Kanisa pamoja na kusisitiza msimamo wa Vatikani.
Miongoni mwa maaskofu wa Amerika ya Kusini ambao walishiriki au kuwemo kwenye Baraza la Pili la Vatikani mwaka 1962 hadi mwaka 1966 ambao wanaonekana kuwa ndio msingi wa kile kilichokuja kujulikana kama Nadhari ya Ukombozi karibu hakuna yoyote aliyebakia katika ngazi ya juu ya Vatikani hivi leo na ni watano tu kati ya makadinali 135 walioteuliwa hawakuchaguliwa na papa.
Nchini Brazil na Mexico nchi mbili ambazo zina wafuasi wengi wa dhehebu la Katoliki na ambapo Papa alizitembelea zaidi ya mara nne ni maaskofu wachache tu wenye kupendelea mageuzi wamebakia katika ulimwengu wa kanisa.
Jose Oscar Beozo mwandishi wa historia ya taathira ya mapapa kwa Brazil anaamini kwamba Vatikani imefanya kosa kwa kuitatanisha Amerika ya Kusini na Ulaya ya Mashariki juu ya kwamba baadae papa alibadili mwendo wake na kuanza kuushutumu ubepari wa kishenzi na utandawazi wa kiuchumi usiokuwa na udhibiti.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya Nicaragua hapo mwaka 1983 mbele ya watu 700,000 Papa John Paul wa Pili aliishutumu serikali ambayo ilikuja kuundwa baada chama cha Sandinista kuushinda udikteta wa Somoza lakini hakusema chochote juu ya Contra wanamgambo waliokuwa wakigharamiwa na Marekani ambao walijaribu kuuangusha utawala wa Sandinista.Wanicaragua wengi walijibu kauli zake hizo kwa makelele na kumzomeya. Baadae alipokuweko Chile na Argentina papa hakusita kutowa chakula cha bwana kwa madikteta wa kijeshi na kugusia kidogo tu ju ya ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu uliotokea katika nchi hizo kwenye miaka ya 1970 na 1980.
Katika mwaka 1996 maadhimisho ya miaka 50 ya ndoa ya aliyekuwa dikteta wa Chile wakati huo Augusto Pinochet ambaye alitawala kuazia 1973-1990 Papa John Paul wa pili na mshauri wake mkuu Nagel Sodano walituma picha ya papa na maalezo yake yenye kumtaja Rais Pinochet na mkewe kuwa ni mfano wa wana ndoa wa Kikristo.
Kufuatia kusambaratika kwa Urusi Papa John Paul wa Pili alianza kushutumu vikali ubepari wa kishenzi unaohodhi kila kitu bila kujali maslahi ya wanyonge wakati wa ziara yake ya Amerika Kusini ambapo aliweka mkazo zaidi kwa haki za kiuchumi na kuheshimiwa kwa haki za binadaamu na hivi karibuni kabisa papa alikuwa akipinga vikali vita viliyoongozwa na Marekani nchini Iraq.
Hakuna mtu anayeweza kusema kwamba Papa hakubadili Kanisa La Katoliki Amerika ya Kusini na kuliondosha kutoka nyendo za mageuzi za miaka ya 1960 na mapema 1970 na kuliweka kwenye mtazamo wa kihafidhina zaidi kiini chake kikiwa ni uokovu wa kiroho.
Litakuwa Kanisa hili jipya la Katoliki ambapo hapo leo litasherehekea miaka 25 ya tokea Wojtyal wa Poland awe papa.
Miongoni mwa maaskofu 135 wana mamlaka ya kumchaguwa mrithi wa Papa John Paul wa Pili na wao wenyewe ni wagombea wa kuwa kiongozi wa kidini wa zaidi ya wafuasi bilioni moja wa dhehebu la katoliki duniani.