Papa Francis anatibiwa homa ya mapafu
20 Februari 2025Taarifa kutoka Makao makuu ya Kanisa Katoliki ya Vatican imesema leo kuwa Baba Mtakafitu alikuwa na usiku mtulivu.
Papa Francis alilazwa hospitali wiki iliyopita baada ya kukumbwa na matatizo ya kupumua, lakini sasa amegundulika kuwa na nimonia katika mapafu yake yote mawili.
Vatican imeripoti kuwa Francis alikuwa na usiku mtulivu, na akaamka vyema na kupata kifungua kinywa. Amekuwa katika hospitali ya Gemelli mjini Rome kwa usiku wa tano mfululizo.
Hapo jana, taarifa ya Vatican ilisema kuwa Francis alikuwa katika hali nzuri, ikiongeza kuwa amekuwa akipumzika na wakati mwingine kusoma vitabu.
Lakini katika matrangazo ya jana usiku, Vatican ilionya kuwa vipimo vya maabara, picha za xray kwenye kifua, na hali ya kiafya ya Baba Mtakafitu viliendelea kuonyesha hali ngumu inayomkabili.
Massimo Andreoni, profesa wa magonjwa ya kuambukiza katika Chuo Kikuu cha Roma Tor Vergata na mkurugenzi wa kisayansi wa Jumuiya ya Magonjwa ya Kuambukiza na Kitropiki ya Italia, anasema kuwa ili kujua jinsi matibabu yake yanavyofanya kazi, ni muhimu kusubiri masaa 24 au 48. "Tuna bakteria tofauti wanaoambukiza wagonjwa, na tunahitaji dawa tofauti kutibu kisa hiki. Na pia, jambo lingine muhimu ni kwamba katika hali hii, ni mgonjwa mzee mwenye zaidi ya miaka 88, na hivyo katika mazingira haya, kuendelea kwa ugonjwa huo nahitaji la matibabu ni vigumu zaidi kuliko kwa wagonjwa vijana."
Papa alikatwa sehemu ya pafu lake la kulia alipokuwa na umri wa miaka 21, baada ya kupata ugonjwa wa pleurisy uliokaribia kumuua.
Vatican imefuta shughuli zote za papa zilizotarajiwa siku ya Jumamosi na kusema kuwa hatahudhuria misa siku ya Jumapili, ingawa bado haijatangaza mipango ya sala yake ya kila wiki ya Angelus, ambayo hufanyika Jumapili saa sita mchana.
Francis, mkuu wa Kanisa Katoliki tangu 2013, alilazwa hospitalini baada ya kutatizika kwa siku kadhaa kusoma maandishi hadharani.
Wakati huo huo, waandishi habari na wapiga picha kutoka kote duniani wamekusanyika nje ya hospitali hiyo huku waumini bilioni 1.4 wa Kikatoliki kote duniani wakisubiri kufahamu afya ya kiongozi wa kanisa lao.
Francis sasa ndiye papa wa pili mwenye umri mkubwa zaidi katika historia. Kama mrithi wa Benedict XVI, amekuwa uongozini tangu Machi 2013.
afp, reuters, dpa