Pakistan yazifungia ndege za India anga yake
24 Aprili 2025Hatua hii ya Pakistan ni ya kulipiza kisasi kwa jawabu la India kuhusiana na shambulizi la wanamgambo lililofanywa sehemu moja ya Kashmir, iliyo chini ya utawala wa India.
Katika taarifa, Pakistan imesema jaribio lolote la kuyazuia au kuyaelekeza India maji ya Pakistan ya mto Indus, litachukuliwa kama kitendo cha vita.
Tangazo hilo lililotolewa na afisi ya waziri mkuu wa Pakistan, linafuatia mkutano wa Kamati ya Kitaifa ya Usalama, siku moja baada ya India kusema kuna watu waliovuka mpaka na kufanya shambulizi siku ya Jumanne, ambapo watu 26 waliuwawa kwa kupigwa risasi na wanamgambo katika eneo maarufu la kitalii.
Polisi ya India ilichapisha ilani ikiwataja washukiwa watatu wa wanamgambo ikisema wawili walikuwa Wapakistani, ila New Delhi haijatoa ushahidi au kutoa taarifa zozote kuhusiana na kuwahusisha watu hao na Pakistan.