Pakistan yazidisha hatua za ulinzi:
23 Novemba 2003Matangazo
ISLAMABAD: Kufuatana na mashambulio ya kigaidi nchini Uturuki, nayo serikali ya Pakistan imeongeza hatua zake za ulinzi. Hatua hizo za usalama zimeongezwa katika jumla ya miji 11 mikubwa, yaliarifu magazeti ya Kipakistani. Serikali za mikoa zimekabidhiwa orodha ya majina ya viongozi wa kigaidi wanaofanyiwa taftishi na maafisa wa upelelezi. Pia serikali mjini Islamabad inajiandaa kutangaza marufuku ya kuchapisha vikaratasi na vijitabu vya kidini vinavyotangaza itikadi kali na vita vitakatifu. Siku chache zilizopita vilikwisha pigwa marufuku vyama sita vya itikadi kali nchini Pakistan. - Upande wake Marekani imewafungua wafungwa sita wengine wa Kipakistani kutoka jela yake ya mahabusi katika kituo cha kijeshi cha Guantanamo, kisiwani Kuba. Kwa jumla wamekwisha funguliwa Wapakistani 20 waliokuwa wamewekwa kituoni Guantanamo bila ya kufunguliwa mashtaka yoyote.