Pakistan yaitungua droni ya India eneo la Kashmir
29 Aprili 2025Pakistan imesema imeitungua droni ya India katika mpaka wa eneo la Kashmir. Hayo yameripotiwa na radio ya taifa leo, ikiwa ni wiki moja tangu shambulizi la umwagaji damu dhidi ya raia katika eneo hilo linalozozaniwa.
Jeshi la India pia limesema pande zote mbili zimeshambuliana kwa risasi kwa usiku wa tano mfululizo katika vituo vya upekuzi vya eneo lenye ulinzi mkali katika mlima wa Himalaya.
Hakukutolewa maramoja tarifa za kuthibitisha makabiliano hayo ya risasi lakini radio ya Pakistan imeripoti kwamba jeshi limeitungua droni ya India likisema kilikuwa kitendo cha ukiukaji wa uhuru na kuingiliwa kwa anga lake.
China kupitia msemaji wa wizara yake ya mambo ya nje Guo Jiakun, imezitaka India na Pakistan zisuluhishe matatizo yao kwa njia ya mazungumzo. "India na Pakistan ni nchi muhimu Asia ya Kusini. Kuishi kwao kwa maelewano ni muhimu kwa amani, uthabiti na maendeleo ya eneo hilo. Kama jirani wa India na Pakistan, China inatoa wito kwa pande zote mbili zijizuie na zishughulikie ipasavyo tofauti zao kupitia mdahalo na mashauriano; na kwa pamoja kudumisha amani ya kikanda, utulivu na uthabiti."
Mahusiano kati ya India na Pakistan yamevurugika baada ya India kuituhumu Pakistan kuunga mkono shambulizi katika eneo la India la Kashmir mnamo Aprili 22 ambapo wanaume 26 waliuwawa.
Uingereza imesema Jumanne kwamba inafanya wajibu wake kuhakikisha mvutano hauzidi kutokota kati ya India na Pakistan.