Pakistan yaituhumu India kupanga kuishambulia
30 Aprili 2025Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Pakistan, mamlaka nchini humo zilisema zimekusanya taarifa sahihi za kiintelijensia ambazo inaonesha kwamba India inapanga kuchukuwa hatua ya kijeshi dhidi yake ndani ya kipindi cha masaa 24 hadi 36 yajayo kwa kisingizio cha kile Islamabad inachosema ni tuhuma zisizo msingi kwamba Pakistan ilihusika na mashambulizi ya Pahalgam ya wiki iliyopita.
Hakukuwa na taarifa rasmi kutoka India juu ya uwezekano wa mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Pakistan, lakini tayari maafisa wa serikali walikuwa wamesema kuwa Waziri Mkuu Narendra Modi alishatoa uhuru kamili kwa jeshi kuamuwa juu ya njia, shabaha na muda wa India kujibu mauaji hayo ya Pahalgam.
Soma zaidi: Pakistan yadai kuwa India inajiandaa kuishambulia wakati mvutano wao ukiongezeka
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alifanya mazungumzo kwa nyakati tafauti na mawaziri wakuu wa India na Pakistan, akisisitiza haja ya kukwepa makabiliano ambayo yanaweza kuleta maafa makubwa.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani pia imetowa wito wa pande hizo mbili kujizuwia na imesema waziri wake, Marco Rubio, angelizungumza na mawaziri wa mambo ya kigeni wa India na Pakistan.
Uhasama waongezeka, India yawafukuza raia wa Pakistan
Hatua ya India kutaka kuiadhibu Pakistan baada ya kuishutumu kuunga mkono mashambulizi ya Pahalgam zimeufanya mvutano kati ya mahasimu hao wawili wenye silaha za nyuklia kufika kiwango cha juu kabisa tangu mwaka 2019, pale pande hizo mbili zilipokaribia kuingia vitani kufuatia mashambulizi ya kujitowa muhanga katika eneo hilo hilo la Kashmir.
Katika mashambulizi ya wiki iliyopita, watu wenye silaha kuwauwa raia 26, wengi wao watalii wa India, karibu na mji wa kitalii wa Pahalgam pia katika eneo hilo hilo la Kashmir linalowaniwa na pande hizo mbili.
Soma zaidi: Pakistan yaitungua droni ya India eneo la Kashmir
Hayo yakijiri, muda wa mwisho uliotolewa kwa raia wa Pakistan kuondoka nchini India umepita tangu Jumapili, huku familia nyingi zikiwa bado zinawania kuvuuka mpaka kwenye mji wa Attari, kaskazini mwa jimbo la Punjab.
Mashuhuda wanasema baadhi ya raia hao wa Pakistan wamefika mpakani hapo kwa hiyari yao, lakini wako wengi walioburuzwa hapo na polisi ya India.
Mmoja wao, Sara Khan, mwanamke wa Kipakistani aliyelazimishwa kuondoka bila mumewe, Aurangzeb Khan mwenye paspoti ya India, aliliambia shirika la habari la AP kwamba amelazimishwa kuondoka.
Soma zaidi: Vikosi vya India na Pakistan vyashambuliana katika jimbo la Kashmir
"Tumehamia na familia zetu hapa. Tunaiomba serikali isizisambaratishe familia zetu. Wananiambia mimi ni haramu kwangu kukaa hapa na lazima niondoke." Alisema mwanamke huyo aliyekuwa na mtoto wake mwenye umri wa wiki mbili tu mkononi, ambaye amekuwa akiishi upande wa Kashmir unaodhibitiwa na India tangu mwaka 2017.