Pakistan yafanya jaribio la pili la kombora la masafa marefu
5 Mei 2025Taarifa ya Pakistan iliyotolewa hivi leo imeeleza kuwa jeshi la nchi hiyo limefanya jaribio la kombora lenye uwezo wa kusafiri umbali wa kilomita 120. Hilo ni jaribio la pili katika muda wa siku mbili. India inaishutumu Pakistan kwa kuhusika na shambulio baya dhidi ya watalii katika eneo lake la Pahalgam huko Kashmir, tuhuma ambazo zimekuwa zikikanushwa na serikali ya Islamabad na kutaka uchunguzi huru ufanyike.
Pakistan imelisifu jeshi lake kwamba liko imara na kusisitiza kuwa majaribio hayo yanalenga kuhakikisha kuwa wanajeshi wako tayari na kuthibitisha iwapo vigezo muhimu vya kiufundi vimekamilika na kwamba silaha hizo zinaweza kutumiwa kwa usahihi. Siku ya Jumamosi, jeshi la Pakistan lilisema lilifanya jaribio ya kombora lenye uwezo wa kusafiri kilomita 450 bila hata hivyo kutoa maelezo zaidi. Mzozo kati ya India na Pakistan unaendelea kufukuta baada ya shambulizi la mwezi uliopita katika eneo linalozozaniwa la Kashmir.
Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif amesema katika taarifa kuwa ameridhishwa na "maandalizi kamili ya jeshi kwa ulinzi wa taifa, akisisitiza kuwa kufanikiwa kwa majaribio hayo kunaonyesha wazi kwamba ulinzi wa Pakistan uko kwenye mikono salama." Sharif ameahirisha ziara yake iliyopangwa kufanyika Ijumaa nchini Malaysia kutokana na kuongezeka kwa hali ya wasiwasi kufuatia mvutano huo.
Soma pia: India yapiga marufuku bidhaa zinazotoka au kupitia Pakistan
Muhammad Luqman ni mkazi wa Kashmir upande wa Pakistan na amerejelea kauli ya Waziri Mkuu: "Hatuna wasiwasi wowote. Tunajihisi tuko salama kama tulivyokuwa kabla ya mivutano hii. Sababu ni kwamba tunaamini ulinzi wa nchi yetu uko kwenye mikono salama. Kwa hivyo hatuna hofu ya aina yoyote."
Hatua za India na jaribio la upatanishi la Iran
Harakati hizi za Pakistan zinashuhudiwa baada ya Waziri Mkuu wa India Narendra Modi kusema wiki iliyopita kuwa amewapa wanajeshi wake "uhuru kamili wa kufanya kazi" ili kujibu shambulio la Aprili 22 huko Pahalgam ambalo liliua watu 26. Na baadaye Pakistan ilisema inazo taarifa za kuaminika za kiitelinjesia kwamba jirani yake huyo anajiandaa kuwashambulia na kuahidi kujibu vikali shambulizi lolote.
Hayo yakiarifiwa, Iran imemtuma leo Jumatatu waziri wake wa mambo ya nje Abbas Araghchi huko Pakistan ili kujaribu kuyapatanisha mataifa hayo jirani na atakutana na mwenzake wa Pakistan Ishaq Dar ambaye amepongeza hatua hiyo ya upatanishi.
Soma pia:India yataka washambuliaji wa Kashmir wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria
Licha ya shikizo la kimataifa kuongezeka dhidi ya India na Pakistan likizitaka nchi hizo kujizuia na hatua zozote za kuuchochea mzozo huo, ziara ya Araghchi ni ya kwanza kufanywa na kiongozi wa kigeni tangu kuanza kwa mvutano huu mpya.
Eneo lenye waislamu wengi la Kashmir linalozozaniwa lina wakazi karibu milioni 15 na limegawanywa sehemu mbili ambazo India na Pakistan kila mmoja husimamia eneo lake, lakini kila mmoja amekuwa akidai kuwa eneo zima la Kashmir ni himaya yake.
(Vyanzo: Mashirika)