Pakistan na Iran zasaini makubaliano ya kiuchumi na usalama
3 Agosti 2025Nchi hizo mbili pia zimejitolea kushirikiana kwa karibu zaidi kukabiliana na tishio la ugaidi kwa manufaa ya amani na ustawi wa kikanda.
Makubaliano muhimu katika sekta mbalimbali, ikiwemo nishati na biashara, yalisainiwa wakati wa ziara ya siku mbili ya Rais wa Iran Masoud Pezekshian mjini Islamabad.
Viongozi wa nchi hizo mbili pia wameahidi kuutatua mzozo wa muda mrefu kuhusu mradi wa bomba la gesi la Iran - Pakistan ambao umekwama kwa zaidi ya miaka 10 kutokana na vikwazo vya kimataifa.
Makubaliano hayo yanaashiria kuimarika kwa uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Iran na Pakistan.
Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Shariff amesisitiza msimamo wa nchi hiyo wa kuunga mkono haki ya Iran ya kuendeleza mpango wa nyuklia kwa matumizi ya amani chini ya mkataba wa Umoja wa Mataifa na kulaani uchokozi wa Israel dhidi ya Iran, kwa kusema "hakuna msingi wowote wa kuhalalisha hilo."