Pakistan na India zafikia makubaliano ya kusitisha mapigano
10 Mei 2025Pande zote zimethibitisha kuwa makubaliano hayo sasa yameanza kutekelezwa mara moja. Rais Donald Trump amesema makubaliano hayo ya kusitisha mapigano kati ya India na Pakistan yamefikiwa kutokana na upatanishi wa Marekani. Pakistan hata hivyo imesema kuwa Saudi Arabia na Uturuki zilishiriki pia mchakato wa upatanishi.
Kufuatia hatua hiyo, Pakistan imetangaza pia kuifungua anga yake na kuruhusu safari zote za ndege.
Mapema siku ya Jumamosi, Pakistan na India zimeendelea kushambuliana usiku wa kuamkia Jumamosi na ´kutunishiana misuli´, licha ya kutangaza kuwa tayari kupunguza mvutano kati yao.
Serikali ya Pakistan ilisema raia 13 wameuawa katika upande wake kwenye eneo linalozozaniwa la Kashmir. Jumuiya ya kimataifa imezitaka nchi hizo mbili zenye silaha za nyuklia kujizuia kuutanua mzozo huo. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio amezitolea wito India na Pakistan kuzungumza ili kuepuka kuzusha vita kamili.
Soma pia: Pakistan yasema India imeziburuza nchi hizo karibu na mzozo mkubwa
Mvutano huu mpya ulizuka Aprili 22 mwaka huu kulipotokea shambulio huko kwenye mji wa Pahalgam, eneo maarufu la watalii huko Kashmir na kusababisha vifo vya watu 26. India inaituhumu Pakistan kuhusika na shambulio hilo, jambo ililolikanushwa vikali.