Pakistan kupinga kusitishwa kwa mkataba wa maji na India
29 Aprili 2025Waziri wa sheria na haki wa Pakistan Aqeel Malik, ameiambia Reuters kwamba siku ya Jumatatu, nchi yake ilikuwa inafanyia kazi angalau machaguo matatu ya kisheria, ikiwa ni pamoja na kuwasilisha suala hilo kwenye Benki ya Dunia iliyosimamia mkataba huo.
Mzozo wazidi kufukuta kati ya India na Pakistan baada ya shambulio Kashmir
Malik amesema Pakistan ilikuwa inafikiria kuchukua hatua katika Mahakama ya Kudumu ya Usuluhishi au katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ huko The Hague ambako inaweza kupeleka madai kwamba India imekiuka Mkataba wa Vienna wa Sheria ya Mikataba ya mwaka 1960.
Pakistan yakaribia kukamilisha maamuzi ya hatua za kisheria
Waziri huyo ameongeza kuwa mashauriano ya mkakati wa kisheria yanakaribia kukamilika na kwamba uamuzi kuhusu masuala yatakayofuatiliwa utafanywa hivi karibuni na huenda ukajumuisha zaidi ya njia moja.
Hata hivyo, maafisa wa rasilimali za maji waIndia, hawakujibu mara moja ombi la kuzungumzia suala hilo.
Yaliomo kwenye mkataba wa maji kati ya India na Pakistan
Mkataba huo ni makubaliano ya usambazaji na matumizi ya maji kutoka Mto Indus na vijito vyake, ambapo 80% hutumika kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na nishati inayotokana na maji nchini Pakistan. Mkataba huo umekuwa ukizingatiwa hadi sasa licha ya vita na mivutano mingine kati ya mataifa hayo mawili.
Vikosi vya India na Pakistan vyashambuliana Kashmir
Lakini wiki iliyopita, India ilisimamisha mkataba huo wa Indus uliosimamiwa na Benki ya Dunia baada ya shambulizi huko Kashmir, na kusema hali hiyo haitabadilika hadi pale Pakistan itakapoacha kuunga mkono ugaidi wa kuvuka mpaka.
Pakistan imekanusha kuhusika kwa namna yoyote katika shambulizi hilo lililosababisha vifo vya watu 26.