Operesheni za kijeshi zaendelea Pakistan kuwasaka magaidi
20 Machi 2004Matangazo
ISLAMABAD: Wanajeshi wa Pakistan wameendeleza operesheni zao za kuwasaka magaidi wa chama cha Al Qaida. Helikopa za kijeshi zilishambulia vituo vya majabalini katika eneo la Waziristan ya Kusini kwenye mpaka wa Afghanistan. Inashutumiwa kuwa huko wamejizatiti zaidi ya magaidi 400 wa itikadi kali. Pia kiongozi wa pili wa Al Qaida, Mmisri Aiman as Sawahiri anashutumiwa kuweko katika eneo hilo. Navyo vikosi maalumu vya Kimarekani na Kiingereza vinaendeleza operesheni zao za kumtafuta Bin Laden nchini Afghanistan. Magazeti ya Kiingereza yameripoti kuwa serikali mjini London imepeleka mabingwa wake 100 katika eneo hilo ikiitika mwito kutoka Marekani. Inasemekana Rais wa Marekani George W. Bush anahimiza kwamba mkuu huyo wa Al Qaida atiwe nguvuni kabla ya Mei. Kama si hivyo wapinzani wake katika kampeni ya uchaguzi wanaweza kumshutumu kuwa hajawatia mbaroni magaidi walioandaa mashambulio ya Septemba 11.