Operesheni ya uokoaji baada ya utekaji nyara Pakistan
12 Machi 2025Vyanzo vya usalama vimesema 155 kati yao wameachiliwa katika saa 24 zilizopita. Zaidi ya abiria 450 walikuwa kwenye treni hiyo ilipokamatwa na wanamgambo na idadi isiyojulikana ya mateka bado wanashikiliwa.
Wanamgambo walishambulia kwa mabomu sehemu ya njia ya reli na kuvamia treni hiyo jana alasiri katika mkoa wa Balochistan, unaopakana na Iran na Afghanistan, ambapo mashambulizi ya watu wanaotaka kujitenga yamekuwa yakiongezeka.
Kulingana na vyanzo vya usalama, "magaidi wamewaweka washambuliaji wa kujitoa mhanga karibu na abiria wasio na hatia ambao wanashikiliwa mateka". Inaripotiwa kuwa magaidi 27 wameuwa katika makabiliano na vikosi vya usalama.
Abiria walioachiwa huru wameeleza jinsi walivyotembea kwa saa nyingi kwenye maeneo ya milimani ili kuwa salama. Kundi la Baloch Liberation Army - BLA limedai kuhusika na shambulizi hilo.