OPEC+ yakubaliana kuongeza uzalishaji wa mafuta
3 Agosti 2025Hatua hiyo ya kuongeza uzalishaji wa mafuta inatokea wakati hofu ikiongezeka kuhusu changamoto za usambazaji wa mafuta na pia kama sehemu ya kukabiliana na mahitaji yanayoongezeka.
Uamuzi wa mwisho unatarajiwa kutolewa katika mkutano uliopangwa kufanyika baadae leo, katikati ya shinikizo linaloongezeka kutoka kwa Marekani kwa serikali ya India kusitisha ununuzi wa mafuta ya Urusi – kama sehemu ya juhudi za Washington kuishinikiza Moscow kukaa kwenye meza ya mazungumzo ya amani na Ukraine.
Muungano wa OPEC+ unajumuisha pia nchi nyingine 10 zinazozalisha mafuta kwa wingi japo sio wanachama wa muungano huo, ikiwemo Urusi na Kazakhstan. Iwapo makubaliano ya kuongeza uzalishaji yatafikiwa, itaashiria kwenda kinyume na sera ya awali kuhusu uzalishaji na inaweza kuwa na athari kubwa kwa bei ya mafuta duniani.
Muungano huo ambao huzalisha karibu nusu ya mafuta duniani na wenye ushawishi mkubwa katika bei ya mafuta, umekuwa ukipunguza uzalishaji kwa miaka kadhaa ili kuwa na utulivu wa bei katika soko la mafuta duniani.