Oparesheni ya jeshi la Marekani dhidi ya waasi nchini Iraq
9 Mei 2005Hatua hiyo imekuja baada ya kuongezeka kwa mashambulio ya mabomu yanayofanywa na waasi kuihujumu serikali mpya ya Iraq.
Wanajeshi wa Marekani pamoja na mabaharia wakitumia ndege wamefanya oparesheni hiyo katika eneo la mkoa wa magharibi wa Anbar.
Taarifa ya jeshi la marekani nchini humo inasema idadi ya waasi waliouwawa kwenye oparesheni hiyo katika kipindi cha masaa 24 imefikia 75.
Oparesheni hiyo dhidi ya waasi na wapiganaji kutoka nje ya Iraq imekuja baada ya kufanyika mashambulio mabaya ya mabomu ambapo majeshi ya Marekani yaliuwawa.
Siku ya jumapili wanajeshi watatu wa Marekani waliuwawa katika mashambulio mawili tofauti ya mabomu yaliyokuwa yametegwa kando kando ya barabara huku mwanajeshi mmoja akiuwawa kwa kupigwa risasi.
Waasi nchini Iraq wamezidisha mashambulizi dhidi ya vikosi vya usalama vya nchi hiyo pamoja na wanajeshi wa Marekani tangu kutangazwa kwa serikali mpya ambapo baadhi ya nyadhifa za mawaziri zilisalia wazi huku takriban watu wasiopungua 300 wakiuwawa katika mashambulio ya kujitoa muhanga na mabomu.
Wakati siku zinazidi kuyoyoma wairaq wengi walidhani baada ya kupita wingu zito la mashambulizi wekendi iliyopita na kutajwa kwa majina sita ya mawaziri waliokuwa wamesalia kuchukua nyadhifa zao huenda kukajaza pengo la kisiasa ambalo limedhaniwa kuongeza mashambulio ya waasi lakini waziri mmoja amekataa kuchukua wadhifa aliopewa huku akisababisha serikali hiyo kubakia tena na pengo.
Bwana Hisham Al Shibli ambaye alipendekezwa kuchukua wadhifa wa waziri wa haki za binadamu na kuwawakilisha wasunni waliowachache aliukataa wadhifa huo.
Akiutembelea mji mtakatifu wa washia wa Najaf waziri mpya wa mambo ya ndani Bayan Jabor amesema serikali mpya ya Iraq imewakamata magaidi 40 akiwemo kiongozi mkubwa wa kigaidi ambaye bado hajatangazwa jina lakini atatangazwa siku kadha zijazo.
Lakini hata hivyo tangazo hilo halijawaridhisha sana wairaq waliojitokeza kwa ushujaa kupiga kura januari 30 kuwachagua viongozi waliowatarajia kuumaliza mzozo uliosalia kuwa kitendawili.
Maafisa nchini Iraq wanasema kujipanga upya kwa waasi katika kufanya mashambulio huku wanasiasa nao wakichukua muda wa miezi mitatu wakizozana baada ya uchaguzi wa januari 30,kushamiri kwa mashambulio ya waasi katika kipindi cha wiki mbili kumezidisha tabu chungunzima kwa wanasiasa walioahidi kuimarisha nchi hiyo.
Licha ya kuapishwa kwa mara nyingine tena kwa mawaziri wapya hii leo bado kumebakia mgawanyiko wa makabila ambao tangu hapo umekita mizizi katika siasa za Iraq.
Upande mwengine wakati serikali mpya ya Iraq inafanya ajizi kuwakabili waasi,inatia hofu zaidi kwamba mzozo utazidi kuleta mgawanyiko na mwishowe kuitumbukiza nchi hiyo katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.
Juhudi za serikali mpya za kuiweka Iraq kuwa taifa la umoja zinatishiwa na mashambulio ya kila uchao. Katika shambulio la hivi karibuni mshambuliaji wa kujitoa muhanga amejiripua katika kizuizi cha polisi kusini mwa Baghdad na kuwauwa watu wasiopungua watatu na kuwajeruhi wengine wanane.
Rais wa Iraq Jalal Talabani amesema vitendo vya kigaidi pamoja na mashambulio ya waasi yalioanza miaka miwili iliyopita yanayoongozwa na Abu Musab Al Zarqawi yanafadhiliwa na makundi fulani ya kiislamu nchini Saudi.
Talabani ameliambia shirika la habari la Reuters katika mahojiano kwamba
Anaamini hata hivyo Zaqawi ameishiwa nguvu na amekataliwa na wairaq kwa hivyo hakuna tena hofu ya kuzuka vita vya wenye kwa wenyewe nchini Iraq.
Kiongozi huyo wa kikurdi aliyeapishwa mwezi uliopita kama rais wa kwanza asiye mwarabu katika taifa hilo kiarabu amesema Zarqawi anaungwa mkono na watu wenye siasa kali kutoka eneo hilo na wanapata msaada kutoka kundi la Al Qaeda na kutoka kwa wafadhili wengine miongoni mwa baadhi ya makundi ya waislamu wenye siasa kali kutoka mataifa ya nje ambayo hakutaka kuyataja kwa majina.
Wakati huo huo wanajeshi wa Marekani wamesema vikosi vya usalama vya Iraq vimewatia mbaroni waasi wapatao 154 katika kipindi cha siku tatu zilizopita kusini mwa Baghdad.