Ongezeko la magonjwa ya kinywa na meno Tanzania
9 Aprili 2025Wagonjwa wa afya ya kinywa na meno wamekuwa wakipitia kadhia tofauti, kutokana na tatizo husika, akiwemo Christina Chonde, ambaye amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya meno. ''Jino langu limetoboka, nashindwa hata kulala likianza kuuma, naumwa hadi sikio, macho, shingo yote kwa sababu ya jino,'' alisema Christina.
Wataalamu wa Afya ya Kinywa na Meno wanaeleza kuwa vipo vitu mbalimbali vinavyosababisha magonjwa ya kinywa na meno katika jamii. Dokta Baraka Nzobo, Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia huduma za Afya ya Kinywa na Meno kutoka Wizara ya Afya hapa nchini Tanzania, anasema matatizo ya kinywa na meno Tanzania yanasababishwa na vitu vingi, mojawapo ni watu kutosafisha kinywa vizuri na meno yao kwa kutumia mswaki, hali inayochangia ongezeko la idadi kubwa ya wagonjwa wa kinywa na meno nchini Tanzania.
Harufu mbaya kinywani na namna ya kuiondoa
''Lakini pia kuna vyakula hivi vya sukari, lakini sababu zingine ni matumizi ya pombe na tumbaku kupita kiasi. Bidhaa za tumbaku zote, kuanzia sigara, tumbaku yenyewe, ugoro, shisha, hizi pia zinasababisha kupata saratani za kinywa na magonjwa mengine ya fizi,'' alifafanua Dokta Nzobo.
Yajue maradhi ya mara kwa mara yanayoshambulia kinywa
Daktari Bingwa wa Afya ya Kinywa na Meno, Deus Malundi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini mkoani Mtwara, anasema maradhi ya mara kwa mara yanayoshambulia kinywa ni pamoja na meno kuoza, shambulizi la fizi, na sababu zake ni ulaji na unywaji wa vitu mara kwa mara, huku tatizo la fizi likichangiwa na namna ya usafishaji kinywa kwa kutumia mswaki.
Anasema kinachotokea ni kwamba, ndani ya mdomo, unapoanza kula vyakula vyoyote vile mazingira ya mdomo yanabadilika, yaani inatoka katika hali ile ya kusaidia kinywa na meno inashuka zaidi ya kiwango cha tindikali. ''Sasa kile kiwango cha tindikali kinachotengezwa mdomoni, kinachosababisha meno kuoza. Lakini magonjwa ya fizi yanaathiri watu wengi na bila shaka sehemu kubwa tunasema ni namna watu wanasafisha vinywa, labda hawasafishi vizuri,'' alibainisha mtaalamu huyo wa afya ya kinywa na meno.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya hivi karibuni kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kinywa na Meno, imeeleza kuwa asilimia 76.5 ya Watanzania wenye umri wa kuanzia miaka 15 na kuendelea wameoza meno na asilimia 31.1 ya watoto wameoza meno yao ya utotoni, huku asilimia 68 ya Watanzania wote wakikabiliwa na magonjwa ya fizi.
Asilimia 57 ya watoto wana magonjwa ya fizi, lakini pia kuna changamoto ya mpangilio mbaya wa meno ambao ni asilimia karibia 31 na pia kuna meno ambayo wataalamu wa afya wanasema meno ya kahawia. Inaelezwa kuwa asilimia 36 ya Watanzania, wana changamoto ya meno ya kahawia, na hayo meno ya kahawia yanapatikana sana kwenye mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Singida, Manyara, na baadhi ya maeno ya Rungwe mkoa wa Mbeya.'
Mohammed Sinani pia amekuwa akisumbuliwa sana na matatizo ya meno. ''Nikitafuna chakula haya meno ya chini kidogo yanaleta changamoto, na muda mwingine ufizi unapovimba sipati kabisa usingizi. Yaani nasikia maumivu makali sana,'' alisema Sinani.
Wataalamu wa afya ya kinywa na meno wanahimiza kuwa ni muhimu kufahamu dondoo muhimu ili kutunza kinywa chako, na jambo la kwanza la kulizingatia ni kusafisha kinywa kwa kutumia mswaki mara mbili kwa siku kwa kutumia dawa ya meno yenye madini ya Fluoride, mara baada ya kuamka na usiku baada ya kula chakula.
Pia wanashauri watu wawe wanaenda kwa daktari wa meno kuangalia kama meno yao yana tatizo, angalau mara moja kwa mwaka. Kadhalika unahimizwa kuepuka matumizi ya tumbaku na pombe kwani yanaharibu ubora wa meno na kuchangia harufu mbaya mdomoni.